Kimataifa

Watawa walalamikia kufanyishwa kazi za sulubu Vatican

March 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

VATICAN CITY, ROMA

WATAWA watatu katika makao makuu ya Kanisa Katoliki wamelalamikia kile walichodai ni kudhulumiwa kwa kufanyishwa kazi ngumu na makasisi.

Walisema wakati mwingine wao hufanyishwa kazi za sulubu hata bila malipo.

“Baadhi ya watawa ambao wameajiriwa na makasisi hurauka alfajiri na kuanza kazi ya kupiga deki na kuosha nguo mchana kutwa bila kupumzika. Watatu kati yao walisema wanahisi kuwa hiyo ni dhuluma,” akasema Mtawa Marie, mzaliwa wa Afrika Kusini ambaye aliwasili Roma miaka 20 iliyopita.

Ni muhali kwa watawa kutoka mataifa yanayoendelea kuibua pingamizi kama hizo sababu kazi yao na gharama ya jamaa zao hulipwa na makanisa yao katika mataifa walikotoka.

“Hii ndiyo maana baadhi ya watawa huamua kunyamaza licha ya kupitia maisha magumu mikononi mwa makasisi,” Marie aliliambia jarida la kila mwezi la “Women, Church, Word” ambalo huchapishwa jijini Vatican.

Mnamo 2016, Papa Francis aliwashauri watawa kuibua malalamishi endapo wanalazimishwa kufanya kazi katika mazingira magumu.

Mtawa Marie alielezea masaibu yake katika jarida hilo akiandamana na wenzake, Paule na Cecile.

“Watawa hufanyishwa kazi bila utaratibu wowote na nyakati zingine hupewa malipo duni. Isitoshe, kuna nyakati ambapo baadhi yao huhudumu bila malipo,” akasema

Mtawa Marie alieleza kuwa inakasirishwa na makasisi ambao huwadharau watawa ambao huwafanyia kazi.