Wachoshwa na genge la Sangwenya, wamtaka Matiang'i aliangamize
Na WANDISHI WETU
VIONGOZI kutoka Kaunti ya Migori sasa wanamtaka waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i kukabiliana na genge la Sangwenya ambalo limekuwa likiwahangaisha wakazi wanaoonekana kupinga serikali ya kaunti.
Genge la Sangwenya limekuwa likihusishwa na gavana Okoth Obado ambaye amejitokeza na kujitenga nalo.
Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed amekuwa mstari mbele kulaani mambo yanayotekelezwa na kundi hilo.
“Juhudi zetu za kuwataka polisi kuwachukulia wafuasi wa kundi hili hatua za kisheria hazijafua dafu. Wakazi sawa na baadhi ya wafanyakazi katika serikali ya kaunti ya Migori wamekuwa wakitishwa na hata kuvamiwa na wafuasi wa genge hilo,” alisema Bw Mohamed katika mahojiano na Taifa Leo.
Katika kaunti za Kisii na Nyamira, usalama hudumishwa hasa na wanachama wa kundi haramu la Sungusungu.
Kutamkwa tu kwa jina hilo husababisha hofu kubwa kwa baadhi ya wakazi huku wengine wakilishukuru kwa kurejesha na kudumisha amani katika kaunti hizo.
Nao wakazi wa Kisumu sasa wanalalama kuwa genge la 42 Brothers lililosambaratishwa na polisi miaka miwili iliyopita, sasa limerejea na limeanza kuhangaisha watu katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo.
Genge hilo liliibuka jijini Kisumu mnamo 2015 na lilishutumiwa kwa kutekeleza mauaji na kubaka waathiriwa.
Genge hilo linadaiwa kuwa hatari zaidi kuliko magenge mengine kama vile Chinese na American ambayo pia yamekuwa yakihangaisha watu jijini Kisumu. Mitaa iliyoathiriwa zaidi na magenge ni Nyalenda, Kondele, Bandani, Obunga na Nyawita.
Katika Kaunti ya Homa Bay, polisi katika eneobunge la Suba Kusini, walinasa washukiwa wawili waliokuwa wamevalia sare za jeshi wiki iliyopita wanaoaminika kuwa wafuasi wa genge linalofahamika kama Big Brothers ambao wamekuwa wakihangaisha wakazi wa mji wa Sindo.
Imeripotiwa na RUTH MBULA, VICTOR OTIENO na GEORGE ODIWUOR