Makala

MBURU: Ni wazi, viongozi wa wafanyakazi hawana haja nao

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

HUKU hali ya maisha kwa Wakenya wa kawaida ikizidi kuharibika kila siku kutokana na mzigo mkubwa wa ushuru na gharama ya juu ya maisha, yalikuwa matarajio ya wengi kuwa Jumatano, wakati taifa liliadhimisha sikukuu ya wafanyakazi, maslahi ya wafanyakazi yangepewa kipau mbele.

Wakenya wengi walitarajia kuwa viongozi wa wafanyakazi wangetumia fursa hiyo ambayo huja mara moja kwa mwaka kuwatetea kwa nguvu zote, kwani sasa wamesukumwa hadi kwenye ukuta.

Hata hivyo, uongozi wa wafanyakazi ukiongozwa na Katibu Mkuu wa miungano ya wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli uliwachezea wafanyakazi shere, wakati walitumia nguvu nyingi kupiga siasa ambazo haziwasaidii Wakenya kurahisisha ugumu wa maisha, badala ya kutumia nguvu hizo kuwatetea.

Ni hulka ambayo inajijenga nchini, ambapo viongozi wa wafanyakazi nchini wanaonekana kuegemea upande wa siasa na kuasi majukumu yao ya kuwatetea wafanyakazi masikini ambao kila siku kwao maisha ni kung’ang’ana.

Ina maana gani kugeuza siku ya pekee ambayo wafanyakazi wanafaa kupewa habari njema kuhusu jinsi utetezi wa maslahi yao unaendelea, na badala yake kusimama kuanza kutumia lugha ya matusi na kupiga siasa?

Wafanyakazi walikuwa wakitarajia kusikia ikiwa wangepandishiwa mishahara, kutetewa kutokana na kukatwa mishahara kufadhili mambo yasiyoeleweka kama mradi wa ujenzi wa nyumba, pamoja na masuala mengine ya maslahi ya kikazi.

Lakini kwa Bw Atwoli kutumia siku hiyo kuwapa wanasiasa fursa za kusifu muafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na kuzungumza mambo kuhusu referenda na jinsi Rais hafai kustaafu, Atwoli aliwasaliti mamilioni ya wafanyakazi, ambao pesa zao zinakatwa kumlipa ili awatetee.

Leba Dei ya mwaka huu imetoa ishara kuwa wakati wa wafanyakazi kuwaza tena kuhusu nani anayewawakilisha kwa kweli umefika, kwani hakuna siku siasa zitawapelekea chakula mezani.

Wafanyakazi sasa wanaelekea kukata tamaa kutokana na pesa nyingi ambazo wanakatwa na serikali, kila mwezi wakiachwa na pesa chache mno za kujiendeleza kimaisha, huku nao viongozi ambao waliwachagua kuwatetea badala ya kufanya hivyo wakigeuka na kuanza kuimba wimbo wa serikali.

Viongozi wa wafanyakazi waamue ikiwa wanataka kumfurahisha Rais Kenyatta na kuwa vibaraka wake, ama wanataka kufanya kazi waliyochaguliwa kufanya ya kuwakilisha wafanyakazi wa Kenya.