AKILIMALI: Teknolojia yake imewaletea wafugaji na wakulima raha
Na FAUSTINE NGILA
Akilimali ilipotua katika Kaunti ya Nakuru, eneo la Keringet, ilimkuta Robert Kipkemoi akitoa vibuyu vya maziwa kwenye pikipiki yake, katika kituo cha mashine za kuhifadhi maziwa kwenye baridi.
Kama mchukuzi wa maziwa, Kipkemboi huwa na foleni ndefu ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa ambao husubiri kupata huduma zake za kupeleka maziwa kwa kituo hicho kabla ya adhuhuri.
“Kwa siku moja, mimi husafirisha lita 600 za maziwa,” anasema Kipkemboi, ambaye ni mwanabodaboda eneo hili.
Amewekeza katika biashara ya kusafirisha maziwa kutoka kwa wafugaji hadi kwa kiwanda cha Keringet Foods Limited, shirika ambalo huchemsha na kuhifadhi maziwa.
Wakulima humlipa Sh4 kwa kila lita ya maziwa anayofikisha kituoni.
Lakini yeye hupokea malipo kila mwishoni mwa mwezi kupitia kwa kipochi cha kidijitali; programu ya simu ambayo imewaunganisha wakulima, wauzaji wa dawa za mifugo, wachukuzi, mashirika ya wafugaji na wafugaji wenyewe.
Jackson Rotich ni mmoja wa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa ambao huuza maziwa yao kwa kiwanda cha Keringet Foods Limited, ambacho pia hutumia kipochi hicho cha kidijitali.
Kama wengine, yeye hulipwa mwishoni mwa mwezi kwa maziwa yote aliyouza.
Muda mfupi baada ya maziwa ya wafugaji kufika kwa kiwanda hicho na kurekodiwa, wao hupokea arafa katika simu zao kuwafahamisha kuhusu uuzaji huo.
Rotich, ambaye huuza lita 40 za maziwa kila siku kw akiwanda hicho anasema kuwa wote waliosajiliwa kwa mfumo huo wa kidijitali hulipwa asilimia 90 ya mauzo yao kupitia M-Pesa huku asilimia 10 iliyosalia ikihifadhiwa kama akiba kwenye kipochi hicho.
“Pesa zilizowekwa kama akiba kwa akaunti za wafugaji kwenye programu hiyo haziwezi kutolewa, na badala yake hutumiwa kununua mbegu, lishe ya mifugo, fatalaiza na dawa za kuua wadudu na kuzuia magonjwa kutoka kwa duka ambalo pia limesajiliwa katika mtandao huo,” anaeleza Rotich ambaye amekuwa akiwakama ng’ombe wake kwa miaka mitano.
Alijisajili kwenye programu hiyo Agosti na anakiri kuwa kabla ya uvumbuzi huu, kucheleweshwa kwa malipo ya wafugaji kuliwa kunawalazimisha wafugaji kuuza maziwa yao kwa mawakala wapunjaji.
“Baada ya ujio wa teknolojia hii, kila mfugaji hulipwa kila wiki ya kwanza ya kila mwezi,” anasema mzee huyu ambaye kwa sasa anakama ng’ombe wanne ambao wote humpa lita 32 za maziwa kila siku.
Yeye hupokea Sh28 kwa lita baada ya kuondoa zile Sh4 za uchukuzi.
Wakulima wengi eneo hili sasa wamegeukiwa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na ukuzaji wa viazi tangu Agosti 2018 programu hiyo ilipozinduliwa na kuwavutia kutokana na malipo yake ya moja kwa moja.
Pamela Kosgei, mkulima wa viazi hapa pia huuza mazao yake kupitia kwa programu hiyo.
Anasema kuwa teknolojia hiyo imewafungia nje mabroka na kuwapa wakulima imani ya kuwa na fedha mwanzoni mwa kila msimu wa upanzi.
“Awali, nilikuwa ninauza kuku kununua mbegu za viazi baada ya kutumia hela zote kutokana na mauzo. Lakini sasa nina hela za kuwekeza msimu ukianza, sina shaka tena,” anaelezea mkulima huyu anayekuza viazi kwa shamba la ekari 15.
Jukwaa hili la kidijitali sasa limevutia wakulima wengi hasa wakati huu ambapo benki na programu za mikopo kwa riba ya juu.
Limekuwa suluhu kwa wakulima ambao hawana dhamana ya kuomba mikopo kwa benki, na hutatizika kuandaa mashamba na kupalilia mimea.
Kuhakikisha mashirika ya wakulima yanawalipa wakulima kwa wakati ufaao, Dodore, kampuni inayomiliki kipochi hicho cha kidijitali, huwapa wakulima mikopo.
“Tunakopesha mashirika yaliyojisajili kwa jukwaa letu ili kuhakikisha yawalipa wakulima mapema. Kabla ya kutoa mkopo, tunatathmini mali na mikataba ya wakulima kwa mashirika,” anasema Gidraf Wachira, afisa wa fedha katika kampuni hiyo.
Anaweka wazi kwamba ni lazima wakulima wapokee mafunzo ya uhasibu bora wa usimamizi wa mapato kabla ya kuwasajili kwa programu hiyo.
“Tunawaagiza kutenga asilimia ndogo ya mapato yao kupiga jeki kilimo au ufugaji wao. Wanatoa pesa zao kwenye maduka ya dawa za mifugo na mbegu yaliyosajiliwa katika programu yetu,” anasema.