• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:55 AM
Everton kuchuana na Kariobangi Sharks hapo Julai jijini Nairobi

Everton kuchuana na Kariobangi Sharks hapo Julai jijini Nairobi

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Everton itazuru Nairobi mwezi Julai kumenyana na mabingwa wa soka ya SportPesa Shield Kariobangi Sharks katika mechi ya kujipima nguvu, klabu hiyo kutoka nchini Uingereza imetangaza Alhamisi.

Taarifa katika tovuti ya Everton inasema kwamba mechi hiyo ya kirafiki itasakatwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani mnamo Julai 7.

Sharks ilichapa Bandari 1-0 katika fainali ya soka ya SportPesa Super Cup jijini Dar es Salaam nchini Tanzania mwezi Januari mwaka huu wa 2019 na kujikatia tiketi ya kushiriki mechi hiyo ya kimataifa dhidi ya timu ya Everton inayodhaminiwa na kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa.

Ziara ya Everton itakuwa ya pili katika eneo la Afrika Mashariki baada ya kufanya safari yake ya kwanza mwaka 2017 kwa mchuano sawa na huo.

Ilizuru Dar es Salaam mwaka 2017 kupepetana na Gor Mahia. Ilichapa miamba hao wa Kenya 2-1 katika ziara hiyo yao ya kwanza kabisa katika eneo la Afrika Mashaiki iliyofanyika mwezi Julai.

Gor na Everton zilikutana tena mwaka 2018, lakini nchini Uingereza katika uwanja wa Goodison Park baada ya Gor kushinda makala ya pili ya soka ya SportPesa Super Cup yaliyofanyika mjini Nakuru nchini Kenya.

Mechi ya Goodison Park ilikuwa ya kwanza kuhusisha klabu kutoka Afrika Mashariki kucheza dhidi ya timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza. Ilisakatwa mwezi Novemba, huku Gor ikidhalilishwa 4-0.

Alan McTavish, Mkurugenzi wa Mauzo wa Everton FC, amenukuliwa na tovuti ya klabu hiyo akisema, “Tunafurahi sana kuwa tutakuwa tukirejea barani Afrika tena kuchuana na Kariobangi Sharks FC. Tulipokelewa vyema sana tulipozuru Tanzania mwaka 2017 na tunasubiri kwa hamu kubwa kuwa nchini Kenya na tunajua itakuwa ziara ya kufana uwanjani Kasarani.”

“Jinsi ilivyokuwa katika safari yetu iliyopita katika eneo la Afrika Mashariki, tutakutana na jamii za eneo hilo na pia mashabiki na marafiki wetu kutoka SportPesa na tutakuwa tukijifunza mengi kuhusu nchi hiyo na nafasi tunazoweza kupata kutoka eneo hilo.”

You can share this post!

TAHARIRI: Wadau waungane kudhibiti maambukizi ya HIV

Magenge hatari yalivyoteka nchi

adminleo