Habari Mseto

Aua mtoto kwa kupoteza Sh135

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

POLISI eneo la Mwea Mashariki wanamsaka mwanamume ambaye alimuua mwanawe wa miaka mitano kwa kukosa kurejesha Sh135, baada ya kutumwa dukani.

Bintiye mwanamume huyo wa miaka saba aliponea kifo kwa tundu la sindano alipokuwa akijaribu kumuokoa nduguye kutokana na kichapo cha baba yao. Mtoto huyo sasa amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kimbimbi.

Chifu wa kata ya Murinduko Joseph Kariuki alisema kuwa mwanamume huyo wa miaka 36 alimtuma mtoto huyo katika duka la karibu Jumanne saa tisa alasiri, kununua bidhaa za Sh65.

“Wakati mtoto alikosa kurudi na pesa zilizosalia kutokana na noti ya Sh200 alizotumwa nazo, babake alimchapa na kumjeruhi shingoni, majeraha ambayo yalisababisha kifo,” akasema chifu huyo.

Mkewe mshukiwa alirejea nyumbani baada ya kupigiwa simu nyingi na majirani na kuupata mwili wa mwanawe bila uhai, ukiwa umelala sakafuni. Bintiye pia alikuwa amelala sakafuni akiwa amepoteza fahamu.

Tangu wakati huo, mshukiwa ametoweka kijijini, kukwepa ghadhabu za wakazi.

Polisi eneo hilo wamethibitisha kuwa wanamsaka mwanamume huyo, ambaye anafahamika vyema. Kulingana na chifu wa eneo hilo, mshukiwa ambaye ni mfanyakazi wa vibarua kijijini amekuwa akiwachapa mkewe na wanawe mara kwa mara.

Mwili wa mtoto huyo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya Kerugoya, naye dadake anaendelea kutibiwa kutokana na majeraha aliyopokea.