Walioiba katoni 125 za viatu Thika wanaswa Ruiru
Na LAWRENCE ONGARO
MALI ya thamani ya Sh 5 milioni ilinaswa katika nyumba moja mjini Ruiru huku washukiwa wawili wakitiwa nguvuni.
Afisa mkuu wa Polisi katika kaunti ya Kiambu, Bw Ali Nuno Dubat, alisema majambazi wapatao 20 walivamia viwanda viwili, African Leather Industry, na Leather Industry Ltd, mjini Thika ambapo waliweza kuiba viatu katoni 125.
“Wezi hao walifika katika viwanda hivyo mwendo wa saa 2 za usiku huku wakipitia kwa ukuta wa nyuma bila kuonekana. Baadaye waliwafunga kwa kamba walinzi saba waliokuwa ndani ya viwanda hivyo,” alisema Bw Dubat.
Mnamo Jumanne maafisa wa polisi walivamia nyumba moja mjini Ruiru na kuwanasa washukiwa wawili waliopatikana kwenye chumba hicho.
Msako ulipofanywa kuna bidhaa zingine nyingi ziliweza kunaswa kutoka kwenye chumba hicho.
Baadhi ya vitu vilivyonaswa mle ndani ya chumba hicho ni vifaa vya umeme ambazo ni nyaya za stima, shoka na mapanga, mishale na kifaaa cha sefu cha kuhifadhi fedha.
Alisema tayari washukiwa hao wawili bado wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Thika, huku wakiendelea kuhojiwa zaidi kabla ya kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka.
“Kwa wakati huu hatuna mengi ya kusema lakini tunazidi kufanya uchunguzi kwa kuwahoji washukiwa hao wawili ili watueleze mengi kuhusu washukiwa wengine waliovamia viwanda hivyo viwili vya kuunda viatu na kusafisha ngozi mtawalia,” alisema Bw Dubat.
Ametoa onyo kwa majambazi ambao wanamipango ya kuhangaisha watu katika Kaunti ya Kiambu, kuwa serikali iko macho na wako tayari kukabiliana nao wakati wowote.
Meneja wa kiwanda cha African Leather Industry Bw David Mwangi alisema majambazi hao wapatao 20 hivi walivamia eneo lao usiku na kuwafunga kwa kamba walinzi wao 7 ambao walikuwa wakipiga doria mle ndani.
“Sisi tulipata habari ya kwamba majambazi wamevamia eneo hilo na kuvunja afisi kuu ambapo walipekua kila sehemu na kung’oka na fedha, vifaa vya kompyuta na mitambo ya CCTV na kuchukua stakabadhi muhimu,” alisema Bw Mwangi.
Alisema washukiwa hao waliingia na magari matatu yaliyotumiwa kubeba mali walizoiba kutoka viwanda hivyo viwili.
Hata hivyo alisema kuwa hakuna yeyote aliyeumizwa katika uhalifu huo huku washukiwa hao wakiendesha wizi huo bila haraka yoyote.