• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
Kesi ya mauaji ya Ivy yavutia mashahidi zaidi ya 10

Kesi ya mauaji ya Ivy yavutia mashahidi zaidi ya 10

Na TITUS OMINDE

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi, marehemu Ivy Wangeci utawasilisha mashahidi zaidi ya kumi kwa mashtaka yanayomkabili Bw Naftali Kinuthia.

Bw Kinuthia alikanusha mashtaka ya mauaji ya Bi Wangeci aliyedaiwa kuwa mpenzi wake.

Afisa mkuu wa upelelezi katika eneo la Eldoret Mashariki, Bw Ali Kingi alisema asilimia kubwa ya mashahidi hao ni wafanyabiashara ambao wanafanya kazi karibu na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), mahala pa mkasa huo wa Aprili 9.

“Zaidi ya mashahidi 10 wameandikisha taarifa kuhusiana na mauaji ya Ivy ambaye aliuawa kwa kukatwa na shoka na mtu ambaye alidaiwa kuwa mpenzi wake,” alisema Bw Kingi.

Bw Kingi alisema mashahidi hao ambao pia wanajumuisha wanafunzi wamekuwa wakishirikiana vyema na maafisa wapelelezi.

Kinuthia ambaye alisomewa mashtaka baada ya uchunguzi wa akili kubaini yuko timamu kushtakiwa, alikana mashtaka dhidi yake mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu mjini Eldoret, Bw Stephen Githinji mnamo Aprili 30.

Mahakama iliambiwa kuwa Bw Kinuthia alimuua Wangeci mnamo Aprili 9 kwa kumkata shingo kwa shoka karibu na hospitali ya MTRH mjini Eldoret.

Mstakiwa kupitia kwa wakili wake Mbiyu Kamau tayari ameomba kuachiliwa kwa dhamana.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa familia ya marehemu Bi Carolyne Nyakinywa ulipinga ombi hilo.

“Tunapinga ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana, kuna uwezekanao mkubwa wa kugorofisha ushahidi iwapo ataachiliwa mbali na kuhatarisha maisha yake ikiizngatiwa kuwa umma ungali na ghadhabu dhidi yake,” alisema kiongozi wa mashtaka Bi Rosemary Karanja

Mahakama itato uamuzi kuhusu ombi la dhamana mnamo Mei 9.

Kisa hicho kilichovutia hisia kali kitaifa kilitokea wakati ambapo mauaji ya wanawake katika mizozo ya kimapenzi imezidi kushuhudiwa katika maeneo tofauti ya nchi.

Ilisemekana marehemu na mshukiwa walikuwa marafiki tangu utotoni ingawa wazazi wa Ivy walikana madai kwamba wawili hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

You can share this post!

Wabunge wahimizwa kuinua maisha ya vijana wenzao

Raila apongeza kanisa la ACK kwa kukataa pesa za ufisadi

adminleo