MakalaSiasa

JAMVI: Ruto aliepushwa asikutane na Mzee Moi?

May 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA PETER MBURU

Wengi walidhani kuwa huenda ni kutokana na matatizo ya kiafya ambayo Rais huyo Mustaafu amekuwa akikumbana nayo, ndipo alikosa kuhudhuria hafla hiyo, iliyokuwa karibu na nyumbani kwake kabisa.

Hii ni kwa kuwa baada ya habari kutolewa kuwa hafla ingeandaliwa nyumbani kwake Kabarak kabla ya mazishi baadaye Kabimoi, wengi walidhani sababu ilikuwa kumwezesha Mzee Moi kuhudhuria.

Wadadisi sasa wamechukua mtazamo wa kisiasa katika matukio hayo ya mambo, wakihoji kuwa hali ya Mzee Moi kukosa kuhudhuria hafla ya mazishi iliyokuwa karibu na nyumbani kwake lakini baadaye akahudhuria mazishi ambayo yalifanyika mbali, ulikuwa mpango wa aidha kumuepuka ama kuepushwa asikutane na Dkt Ruto.

Naibu Rais amekuwa akizuiliwa kukutana na Mzee Moi na wengi walitarajia kuwa huenda fursa ilikuwa imejitokeza hatimaye, katika mazishi hayo.

Alipokosa katika hafla ya mazishi, wengi walidhani kuwa hangehudhuria mazishi yenyewe, lakini tena wakashangaa kujua kuwa mambo hayakwenda kulingana na matarajio yao.

“Bila shaka huo ulikuwa mpango Mzee Moi wasikae

jukwaa moja ama kukutana na Naibu Rais. Hata Dkt Ruto mwenyewe anataka sana kukutana na Rais huyo Mstaafu na huenda ni sababu hiyo iliyochangia afike mazishini, lakini walihakikisha kuwa hawakutani,” anasema Gilbert Kabage, mdadisi wa kisiasa.

Bw Kabage anaongeza kuwa seneta wa baringo anatumia baraka za babake kupiga hatua kisiasa kwani Mzee Moi anaheshimika katika jamii ya Kalenjin na nchini, hivyo akimzuia Naibu Rais ambaye ni hasimu wake kisiasa kutokutana naye, kwani atatumia fursa hiyo kujipa pia kutafuta umaarufu.

Aidha, baadhi ya wanasiasa wakuu waliokuwa katika hafla ya mazishi hayo Kabarak walikiri kuwa walipitia nyumbani kwa Mzee Moi kumwona asubuhi kabla ya kuhudhuria hafla hiyo.

Matamshi hayo yalionekana kurejesha mjadala kuhusu hali ya baadhi ya viongozi kuzuiwa kumwona Mzee Moi, haswa wandani wa Dkt Ruto, kwani wote waliosema hivyo ni mahasimu wa Naibu Rais.

Kwa upande wao, Dkt Ruto na wafuasi wake hawakusema lolote kuhusu kumtembelea Rais huyo Mustaafu, maneno yao yakiwa kuhusu masuala mengine kabisa.

Baadhi ya viongozi waliokiri kuwa walimwona Mzee Moi na kuzungumza naye siku hiyo ni seneta wa Bungoma Moses Wetangula, seneta wa Siaya James Orengo na spika wa bunge la seneti Kenneth Lusaka.

“Tulikuwa kwa Mzee Daniel Moi asubuhi na kile alichotuambia ni tuchunge maslahi ya Wakenya,” Bw Lusaka akasema alipokuwa akihutubu.

Bw Musyoka naye alisema kuwa siku chache kabla ya hiyo ya mazishi walikuwa wamekutana na Mzee Moi na wakazungumza.

Katika matukio hayo iliibuka kuwa ni Dkt Ruto na wandani wake tu ambao hawakupata fursa ya kumwona Mzee Moi, na hivyo uwepo wa Rais huyo Mstaafu katika mazishi Kabimoi licha ya kukosekana chuo kikuu cha Kabarak likasalia swali miongoni mwa wengi, Mzee Moi aliepuka ama kuepushwa asikutane na Ruto?