Habari Mseto

HUDUMA NAMBA: 'Serikali haina hela za kuongezea watu muda'

May 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI haiko tayari kuongeza muda wa kusajili watu katika mpango wa Huduma Namba jinsi ilivyopanga.

Kamishna wa eneo la kati Bw Wilson Nyangwanga alisema kwa wakati huu serikali haina bajeti ya kulipia siku za ziada.

“Ninatoa mwito kwa wakazi wa eneo la kati wajitokeze kwa wingi ili watekeleze wajibu wao wa kujiandikisha katika mpango huo wa Huduma Namba. Serikali itapata nafasi ya kuweka mikakati maalum jinsi ya kupanga mambo yake baada ya kukamilisha shughuli hiyo,” alisema Bw Nyangwanga.

Aliyasema hayo alipozuru maeneo ya Gatukuyu, Mataara, na Kamwangi mnamo Alhamisi, aliposhuhudia jinsi wakazi wa eneo hilo walivyojitokeza kujiandikisha.

Alisema zoezi hilo ni muhimu sana ambapo hata serikali imepanga pajeti yake wa maafisa hao wanaosajili watu kwa muda huo uliopendekezwa wa siku 45.

Alisema katika eneo la kati serikali inanuia kuwasajili watu wapatao 7 milioni jambo aliyosema itatimia kutokana na jinsi watu wanavyojiandikisha.

Alisema tayari watu wapataaao 2.3 wamejisajili na wanamatumaini katika siku zijazo watafurika kwa wingi kwenye vituo vya kujisajili ili kuepuka kuachwa nyuma ya zoezi hilo.

Alitoa mwito kwa machifu na manaibu wao kufanya bidii kuona ya kwamba zoezi hilo linaendeshwa katika vijiji ili kila mmoja aweze kupata nafasi ya kusajiliwa.

“Wale wanaofaa kushughulikiwa kabisa ni walemavu na wakongwe kwa sababu wengi wao hawawezi kutembea mwendo mrefu hadi kwenye vituo hivyo,” alisema Bw Nyangwanga

Alisema walemavu wanastahili kupewa nafasi ya kwanza kwa vile ni mara nyingi wao husahaulika sana.

Alisema kwa wakati huu wakazi wa Kiambu wapatao 1.3 milioni wamejisajili kati ya watu milioni 3 wanaoishi sehemu hiyo.