• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
Lacazette kubeba Arsenal hadi waingie ndani ya Uefa

Lacazette kubeba Arsenal hadi waingie ndani ya Uefa

Na CHRIS ADUNGO

BAADA ya kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Valencia katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya kuwania ubingwa wa Ligi ya Uropa wiki jana, Arsenal wanapigiwa upatu wa kufuzu kwa fainali ya kipute hicho msimu huu.

Upo uwezekano mkubwa kwa Arsenal kukutana na Chelsea katika fainali ya Ligi ya Uropa baada ya washindani wao hao katika soka ya Uingereza kulazimishia Eintracht Frankfurt ya Ujerumani sare ya 1-1 katika nusu-fainali nyingine ya Alhamisi iliyopita.

Hadi kufikia walipo kwa sasa, Arsenal walipita mtihani mgumu wa Napoli katika hatua ya nane-bora ili kujikatia tiketi ya kuchuana na Valencia ambao ni miongoni mwa miamba wa soka nchini Uhispania.Katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali, Arsenal waliwapepeta Napoli 2-0 uwanjani Emirates kabla ya kuwapokeza kichapo cha 1-0 nchini Italia.

Kwa upande wao, Chelsea waliwakomoa Slavia Prague kutoka Jamhuri ya Czech kirahisi kabla ya kukutana na Frankfurt waliowazidi ujanja Benfica kutoka Ureno.

Chini ya kocha Maurizio Sarri, Chelsea waliwachabanga Arsenal 3-2 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa kampeni za EPL mnamo Agosti 2018.

Hata hivyo, mkufunzi Unai Emery ambaye pia huu ni msimu wake wa kwanza katika soka ya Uingereza, aliwaongoza Arsenal kulipiza kisasi katika mchuano wa mkondo wa pili ligini humo. Mabao kutoka kwa Lacazette na Laurent Koscielny yaliwapa Arsenal ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Chelsea katika marudiano ya EPL mnamo Januari 2019 uwanjani Emirates.

Kikubwa kitakachofanya mwisho wa kampeni za Ligi ya Uropa kuwa wa kusisimua zaidi msimu huu ni ulazima wa Chelsea kukutana na Arsenal katika fainali hasa ikizingatiwa kwamba mmoja wao atamaliza kivumbi cha EPL nje ya mduara wa nne-bora.

Iwapo Manchester United wanaonolewa na kocha Ole Gunnar Solskjaer watamaliza kampeni za EPL ndani ya nne-bora, basi njia ya pekee kwa Arsenal au Chelsea kufuzu kwa kipute cha UEFA msimu ujao ni kunyanyua ubingwa wa Ligi ya Uropa.

Fainali ya kivumbi hicho mwaka huu itaandaliwa ? jijini Baku, Azerbaijan mnamo Mei 29. Ingawa hivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Chelsea wapo pazuri zaidi kutinga mduara wa nne-bora na kuwasaza Arsenal katika nafasi ya tano mbele ya Man-United ambao huenda walaambulia nafasi ya sita.

Iwapo hili litatimia, itamaanisha kwamba Arsenal watasalia na njia moja pekee ya kufuzu kwa UEFA msimu ujao; na njia yenyewe itakuwa ni kuwapepeta Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Uropa.

Chelsea walitawazwa mabingwa wa Ligi ya Uropa kwa mara ya mwisho mnamo 2013 huku Emery ambaye ana historia nzuri katika kivumbi hicho akiwaongoza Sevilla ya Uhispania kunyanyua ufalme wa taji hilo mnamo 2014, 2015 na 2016 mtawalia.

Ilivyo, tumaini la Arsenal la kujitwalia taji la Ligi ya Uropa msimu huu linasalia pakubwa mikononi mwa Lacazette ambaye ushirikiano na urafiki wake na Pierre-Emerick Aubameyang unazidi kuwa nguzo imara kambini mwa kikosi hicho.

Kipaji cha Lacazette katika ulingo wa soka kilitambulika kambini mwa akademia ya Olympique Lyon waliomwajibisha kwa mara ya kwanza kitaaluma akiwa na umri wa miaka 19. Ushawishi wake uwanjani ulikuwa kiini cha Lyon kunyanyua mataji ya Coupe de France na Trophee des Champions mnamo 2012.

Ufanisi huo ulimwezesha kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kambini mwa Lyon mwishoni mwa msimu wa 2014-15. Akiwa mchezaji wa Lyon, Lacazette alijulikana zaidi kwa wepesi wake wa kutikisa nyavu za wapinzani huku akipachika wavuni zaidi ya mabao 20 katika kampeni zote za kipute cha kuwania ufalme wa Ligue 1.

Uwezo wa kukabiliana vilivyo na madifenda, kuwahi mipira ya kichwa, kutamba katika safu yoyote ya uvamizi, kutumia vyema maguu yote mawili na kupiga penalti kwa ufundi mkubwa ni sifa zilizomfanya kuwaniwa na Arsenal mnamo 2017.

Lacazette alirasimisha uhamisho wake hadi ugani Emirates mnamo 2017 kwa kima cha Sh6.5 bilioni. Tangu avalie jezi za timu ya Ufaransa kwa mara ya kwanza, amewakilisha nchi yake katika mashindano yote ya wachezaji chipukizi. Alikuwa tegemeo kubwa kambini mwa Ufaransa katika fainali za Euro 2010.

.kwa matineja wasiozidi umri wa miaka 19. Alisaidia Ufaransa kunyanyua ubingwa wa taji hilo baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Uhispania. Alivalia jezi za kikosi cha kwanza cha Ufaransa mnamo Juni 2013 na kufungua rasmi akaunti yake ya mabao mnamo Machi 2015.

Weledi wa kupiga chenga, uwezo wa kuvurumisha makombora mazito kwa kutumia maguu yote mawili na kasi yake hata awapo na mpira ni baadhi ya sifa zinazowafanya wachanganuzi wa soka kumlinganisha na mafowadi wa zamani wa ? Arsenal – Ian Wright na Gerard Houllier.

Mnamo Oktoba 29, 2016, aliwafungia Lyon mabao mawili dhidi ya Toulouse katika mchuano wa Ligue 1 ugenini na kufikisha jumla ya magoli 101 kapuni mwake kutokana na mapambano yote ndani ya jezi za waajiri wake.

Ni ufanisi uliomfanya kumruka Juninho Pernambucano aliyefunga mabao 100 kutokana na mechi 350. Hadi kufikia sasa, Lacazette anashikilia nafasi ya nne katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika historia ya kikosi cha Lyon.

Licha ya kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Atletico Madrid, Lacazette alijiunga na Arsenal mnamo Julai 5, 2017 kwa mkataba wa miaka mitano. Kuuzwa kwake kuliwavunia Lyon hela nyingi zaidi baada ya kupiku mauzo yaliyotokana na hatua ya Corentin Toliso kujiunga na Bayern Munich mnamo Juni 2017.

Mbali na kuwa miongoni mwa wachezaji ghali zaidi kambini mwa Arsenal, fedha zilizotumiwa na Arsenal kumnunua Lacazette zilizidi zile zilizotolewa kwa minajili ya kiungo Mesut Ozil aliyesajiliwa kutoka Real Madrid kwa Sh6 bilioni mnamo 2013.

You can share this post!

De Bruyne fundi wa soka aliye na hela mfano wa majani ya...

Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kufunguliwa Agosti

adminleo