Habari MsetoSiasa

Si Waititu pekee, bajeti za Ngilu na Oparanya pia zina utata

May 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER MBURU

BAADA ya ripoti kuhusu bajeti tata ya Kaunti ya Kiambu, ripoti sawa zinazidi kujitokeza katika kaunti zingine, nayo afisi ya Mratibu wa Bajeti za serikali ikishikilia kuwa bajeti zilizowasilishwa mbele yake hazikuwa na matumizi ya aina hiyo.

Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu alikuwa na kibarua kigumu kueleza kuhusu sehemu katika bajeti ya kaunti yake mwaka wa 2017/18, ambapo ilinakiliwa kuwa serikali ya kaunti hiyo ilitumia zaidi ya Sh1 bilioni kufadhili shughuli za serikali kuu.

Bajeti ya Kaunti ya Kiambu mwaka jana ilionyesha kuwa, Sh58 milioni zilitumiwa kufadhili mpango wa kutafuta amani Sudan Kusini, Sh973 milioni kufadhili shughuli za ikulu, Sh180 milioni kulipa marais wastaafu marupurupu na Sh804 milioni kugharimia elimu ya bure kwa shule za msingi.

Msimamizi wa Bajeti nchini Agnes Odhiambo, hata hivyo, alisema kuwa bajeti iliyowasilishwa katika afisi yake kuhusu Kaunti ya Kiambu haikuwa na matumizi hayo.

“Matumizi hayo hayakuwa sehemu ya bajeti ya 2017/18 ambayo iliwasilishwa katika afisi ya Msimamizi wa Bajeti na Kaunti ya Kiambu, wala katika bajeti ya ziada,” Bi Odhiambo akasema kupitia msemaji wa afisi yake Stephen Wangaji.

“Matumizi hayo aidha hayakuorodheshwa katika ripoti za kuonyesha matumizi ya pesa kipindi hicho. Kwa hivyo Msimamizi wa bajeti hafahamu kuhusu matumizi hayo,” akasema.

Lakini wakati mkanganyiko huo ukiendelea, ripoti zaidi za Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya pesa za serikali kuhusu serikali za kaunti zimeonyesha kuwa si Kaunti ya Kiambu pekee iliyokuwa na matumizi ya aina hiyo, ila kuna kaunti nyingine.

Kwa mfano, katika Kaunti ya Nyeri ambayo ripoti ya Mkaguzi Mkuu ilionyesha ilitumia pesa vyema, kwenye ripoti kuhusu jinsi ilitumia bajeti yam waka wa 2017/18, Sh197 milioni zilitengwa kugharamia biashara za kimataifa (ambapo Sh150 milioni zililipwa) na Sh910 milioni zikatengwa kugharamia ushauri kwa mashirika ya serikali.

Vilevile, Sh266.3 milioni zilitengwa kugharamia masomo ya shule za msingi, Sh2.07 milioni kugharamia elimu ya shule za msingi bila malipo, Sh264.3 milioni kugharamia masomo ya shule za upili na Sh2.8 milioni kufadhili elimu ya vyuo vikuu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kaunti hiyo aidha ilitumia Sh213 milioni kufadhili maabara ya serikali na Sh138 milioni kufadhili usafiri wa reli, licha ya matumizi hayo yote kuwa ni ya serikali kuu.

Kaunti ya Kakamega nayo kwa mujibu wa ripoti kuhusu jinsi ilitumia bajeti yake mwaka wa 2017/18 ilitenga Sh75 milioni kufadhili shughuli za ikulu (ambapo Sh29 milioni zililipwa), Sh190 milioni kufadhili shughuli za kukusanya takwimu, Sh5.1 bilioni kwa shughuli za ugatuzi (ambapo Sh4.7 bilioni zililipwa) na Sh4.7 bilioni kwa masuala ya ushirikiano kati ya serikali kuu na za kaunti.

Sh124.2 milioni zililipwa kwa ajili ya huduma za utabiri wa hali ya anga, kati ya Sh185.5 milioni zilizotengwa, ripoti hiyo kuhusu Kakamega ikaendelea, nazo Sh18.7 milioni zikatumiwa kufadhili elimu ya shule za upili.

Katika Kaunti ya Kitui, mambo hayakuwa tofauti, Sh60 milioni zikilipwa kufadhili shughuli za ikulu, Sh28 milioni kufadhili utoaji ushauri kwa mashirika ya serikali, Sh79 milioni kugharamia masomo ya shule za msingi na elimu ya shule hizo bila malipo, Sh435 milioni zikitengwa kufadhili masomo ya shule za upili na Sh20.5 milioni masomo ya vyuo vikuu.

Kwa mujibu wa bajeti ya Kitui iliyowasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu aidha, Sh47.3 milioni zilitumiwa kwa utafiti na kuhesabu watu (census), kati ya Sh55.2 milioni zilizotengwa, Sh50 milioni zikalipwa idara ya utabiri wa hali ya anga na Sh270 milioni kufadhili masuala ya sera za kiuchumi na mipango ya kitaifa.

Kaunti hiyo, hata hivyo, haikutumia pesa zozote kufadhili elimu ya chekechea, ambalo ni jukumu la serikali ya kaunti, bajeti hiyo ikasema.

Bajeti hizi zinawaacha watu na maswali tele, haswa kutokana na tofauti za viwango vya pesa zilizorekodiwa kutumiwa katika bajeti hizo na hali kuwa Msimamizi wa Bajeti ameeleza matumizi hayo hayakuwa katika bajeti alizowasilishiwa.

Ikiwa ni kweli kaunti zilitenga bajeti hizo, swali kuu ni Je, ilikuaje Mkaguzi Mkuu akaendelea kutoa ripoti kuwa zilitumia pesa vyema?

Aidha, hali ya Msimamizi wa Bajeti kusema matumizi hayo hayakuwa katika bajeti zilizowasilishwa mbele yake inaibua swali jingine, matumizi hayo yaliingia vipi katika bajeti za kaunti hizo?

Mwisho ni kuwa, ikiwa bajeti zinaonyesha kuwa pesa hizo zilitengwa na magavana kupinga kuwa hawajatumia pesa zozote kwa njia hizo, basi pesa hizo ziko wapi?