Arsenal, Chelsea katika kibarua kigumu Europa
ARSENAL wanaojivunia ushindi wa mabao 3-1 katika mkondo wa kwanza, leo usiku watahitajika kucheza kwa uangalifu ili kuepuka matokeo ya kushtua ambayo huweza kutokea katika mechi hizi za bara Ulaya.
Chelsea ina kibarua kizito kidogo inapoalika Eintracht Frankfurt ya Ujerumani kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza nchini Ujerumani yaliyoisha kwa sare ya 1-1.
Arsenal chini ya kocha Unai Emery wako ugenini uwanjani Mestalla kucheza na Valencia katika marudiano ya nusu fainali ya kuwania ubingwa wa Europa League.
Zilipokutana juma lililopita ugani Emirates, Valencia walitangulia kupata bao la mapema kupitia kwa Alexandre Mouctar Diakhaby, lakini mabao ya Alexandre Lacazette (2) na Pierre-Emerick Aubameyang yaliwaweka katika nafasi nzuri ya kuibwaga Valencia na kufuzu kwa fainali.
Lakini haitakuwa kazi rahisi mbele ya vijana wa kocha Marcelino ambao wameshangaza wengi kwa hatua kubwa waliopiga msimu huu.
Hata hivyo vichapo kutoka kwa Atletico Madrid na Eibar katika mechi za La Liga (Uhispania) vilivyofuata matokeo hayo ya Emirates, kidogo vinawapa wasiwasi mashabiki wao ambao wamesubiri taji hili kwa muda mrefu.
Baada ya matokeo hayo ya kuudhi, Valencia walirejelea ushindi walipoichapa Huesca mabao 6-2 mwishoni mwa wiki, na sasa wengi wanasubiri kuwaona wakibadilisha matokeo dhidi ya Arsenal, leo Alhamisi usiku.
Tatizo kuu kwa kikosi cha Marcelino ni safu ya ulinzi ambayo imekuwa ikilegea mara kwa mara msimu huu katika mechi saba za karibuni ambapo wamekuwa wakifungwa mabao mechi ikielekea kumalizika.
Miongoni mwa wachezaji watakaotegemewa kikosini ni pamoja na aliyekuwa staa wa Arsenal, Gabriel Paulista huku mashambuliaji yakiongozwa na Santo Mina.
Kwa upande mwingine, kufuzu kwa Arsenal kutamfanya kocha Emery atulie baada ya kushambuliwa mara kwa mara na mashabiki wa klabu hiyo.
Hii ndiyo njia nyingine ya mkato kwa klabu hiyo kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa msimu ujao, iwapo wataibuka mabingwa wa taji hili la Europa League.
Fainali ya msimu huu itafanyika mjini Baku nchini Azerbaijan.
Kwenye mechi ya kwanza nchini Ujerumani, Luka Jovic aliifungia Frankfurt bao la mapema ugani Commerzbank-Arena, kabla ya Pedro kuisawazishia Chelsea.
Uefa
Kocha Maurizio Sarri atapanga kikosi chake akikumbuka kwamba ushindi katika mechi utafufua matumaini ya vijana wake kushiriki katika michuano ya UEFA msimu ujao.
Jumla ya mechi 59 zimechezwa kufikia sasa ambapo ushindi kwao utawapa mashabiki wao matumaini makubwa, siku chache tu baada ya Arsenal na Manchester United kushindwa kuandikisha ushindi katika mechi zao za ligi kuu ya Uingereza (EPL).
Ingekuwa kazi rahisi kama vijana wake wangerejea nyumbani na ushindi wa zaidi ya mabao mawili, lakini bao lao la ugenini pia ni muhimu.
Mchezaji nyota, Eden Hazard anatarajiwa kuongoza kikosi cha Sarri baada ya majuzi kuonyesha kiwango cha juu katika ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Watford.
Lakini katika michuano hii ya Europa League, kocha Sarri amekuwa akiwategemea Olivier Giroud na Ruben Loftus-Cheek wakati Hazard akichangia katika kuwapa mipira.
Tatizo kubwa la Chelsea lipo katika safu ya ulinzi baada ya mastaa kadhaa kuumia.
Chelsea ipo katika wakati mgumu kutokana na majeraha yanayowakabili mabeki wake wa kutegemewa katika safu ya kati.