• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
‘Upekee ni sifa muhimu ya utafiti’

‘Upekee ni sifa muhimu ya utafiti’

Na LAWRENCE ONGARO

WAFANYAKAZI  wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) wanaojiendeleza na elimu ya juu walishiriki semina ya uchapishaji na utafiti iliyozinduliwa chuoni humo.

Hafla hiyo iliongozwa na Dkt Bibianne Waiganjo-Aidi ambaye ni Naibu Chansela zingatio likiwa ni kitengo cha utafiti na maswala ya masomo.

Msemaji mkuu katika hafla hiyo alikuwa Profesa Fiona Mbai ambaye ndiye mkurugenzi wa kitengo cha utafiti na ubunifu katika Chuo cha kiufundi cha Technical University of Kenya (TUK).

Katika hafla hiyo ya Jumatano, washiriki walionyesha ujuzi wao unaojiegemeza kwenye maswala mengi ya kidijitali na mambo mengine mengi yanayohitaji maelezo ya ubunifu mpya.

Baadhi ya maswala yaliyotiliwa maanani katika hafla hiyo ni jinsi ya kujieleza kwa kuzingatia utafiti.

Lengo lingine lilikuwa ni kwa kwa nini mtafiti anaendesha utafiti wake na ni kwa lengo lipi?

Jambo jingine ni kwamba utafiti huo una mashiko na unawasilishwa kwa watu gani?

Dkt Ken Ramani alitoa mwito kwa waliohudhuria hafla hiyo kuwa watu wenye maono wanapoendesha utafiti wao.

“Ni sharti kuwa makini na kuona ya kwamba maswala unayoshughulikia yanaambatana na kile unachofuatilia. Na pia lazima uwe na wakati mwafaka wa kukamilisha utafiti wako,” alisema Dkt Ramani.

Walikumbushwa pia kutoingiza kazi ya wengine (plagiarism), bali wajiamini wenyewe na kuandika maoni yao kibinafsi.

Kipaumbele

Walijulishwa pia kwamba utafiti uliofanywa kwa utaratibu unaofaa hupewa kipaumbele; jambo ambalo hufanya mtafiti kuafikia malengo yake kimasomo.

Dkt Ramani aliwajulisha ya kwamba utafiti sio mashindano ya kujigamba eti umemshinda mwenzako, bali huwa ni njia moja ya kubadilishana mawazo kwa kusomo jambo geni kutoka kwa mwenzako.

Alisema hiyo ndiyo maana kuna wataalamu ambao wana ujuzi kamili wa kuelewa iwapo utafiti yoyote ile ina ujumbe wake na mashiko katika muundo wake.

You can share this post!

Konsitebo wakongwe katika kikosi cha polisi roho mkononi

Mtunze mbwa akufae zaidi

adminleo