• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Wabunge wajitengea Sh7b bila kujali wananchi

Wabunge wajitengea Sh7b bila kujali wananchi

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA watazidi kuumia kutokana na ari ya wabunge kujitwalia pesa zaidi bila kujali maslahi ya wananchi.

Sasa wabunge watatumia Sh7.29 bilioni kutekeleza operesheni katika afisi zao maeneo bunge, na kuwalipa wasaidizi wao kuanzia Julai.

Tume ya Huduma za Bunge (PSC) inatafuta kuidhinishwa na wabunge nyongeza ya bajeti ya afisi zao kwa Sh440 milioni kutoka kwa Sh6.8 bilioni wanazopewa sasa.

Wabunge wote 349, maseneta 67 wakiwemo wabunge maalum huajiri wafanyikazi kama vile madereva, makarani, tarishi na wasaidizi wa kibinafsi afisini mwao. Wote hao hulipwa na umma.

Bunge imetengewa Sh6.1 bilioni kwa operesheni katika afisi zao, nayo seneti itatumia Sh1.17 bilioni katika afisi zao za kaunti.

Kulingana na ratiba ya mishahara ya PSC kwa wafanyikazi wa wabunge, wasaidizi wao wa kibinafsi ndio hulipwa zaidi, ambapo kila mwezi hulipwa Sh65, 000. Wale wanaohudumu afisini hulipwa Sh20, 000 kila mwezi.

Wabunge wana uhuru wa kuajiri na kufuta wafanyikazi kama wanavyotaka. Katika mwaka huu wa kifedha, PSC iliwasilisha bajeti ya Sh42.55 bilioni kufadhili wabunge na wafanyikazi wao ila Hazina ya Fedha ilipunguza kiwango hicho hadi Sh38.6 bilioni.

PSC huweka pesa kwa akaunti za operesheni katika afisi za wabunge na maseneta kila baada ya miezi mitatu.

Sasa PSC inatafuta Sh43.6 bilioni kufadhili operesheni katika afisi za viongozi.

You can share this post!

Collymore ateuliwa kwa bodi ya kukabili kansa

Ripoti ya ukaguzi yabashiri kuporomoka kwa ODM bila Raila

adminleo