NYS yaongezewa fedha kwenye bajeti ya ziada
Na CHARLES WASONGA
WIZARA ya Fedha imeongeza fedha kwa Shirika la Huduma ya Vijana Kwa Taifa (NYS) katika makadirio ya bajeti ya ziada yaliyowasilishwa bungeni Alhamisi licha ya kuzongwa na sakata mbili za ufisadi miaka ya nyuma.
Mgao wa fedha kwa NYS uliongezwa kutoka Sh7.8 bilioni hadi Sh12.6 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 60.8.
Katika bajeti ya sasa ya mwaka wa kifedha wa 2018/2019 mgao wa fedha kwa shirika hilo ulipunguzwa kwa Sh8 bilioni katika kile kilichosemekana kuwa hatua ya kukomesha wizi wa pesa za umma.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya maafisa kadhaa wakuu wa shirika hilo na wafanyabiashara wengine kutiwa mbaroni na kufunguliwa mashtaka kwa wizi pesa ambazo upande wa mashtaka ulisema unaweza kutimu Sh10 bilioni.
“Ongezeko hilo linatokana na sababu kwamba NYS ina kiwango kikubwa cha madeni ambayo hayajalipwa. Pesa hizo zitatumiwa kulipia madeni hayo,” akasema Bw Rotich katika makadirio ya bajeti aliyowasilisha bungeni.
Sakata iliyotokea katika NYS mwaka 2018 ilisababisha kufutwa kazi kwa aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Vijana na Utumishi wa Umma Lilian Omollo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai.
Na katika sakata ya kati ya miaka ya 2015 na 2016 ambapo zaidi ya Sh2 bilioni zilipotea katika ununuzi wa bidhaa kinyume cha sheria aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru (sasa Gavana wa Kirinyaga) na aliyekuwa Katibu wa Wizara hiyo Peter Mangiti waliangukiwa na shoka na kuondolewa afisini.
Lakini ajabu ni kwamba mwaka 2018 zaidi ya maafisa 24 wa NYS waliondolewa mashtaka ya wizi wa Sh48 milioni – kosa linalodaiwa kutendwa au kubainika mnamo 2015.
Kuathiri mpango
Kupunguzwa kwa bajeti ya NYS mwaka 2018 kuliathiri mpango wa kutoa vibarua na mafunzo kwa vijana katika mitaa 60 ya mabanda ambayo yaliyotarajiwa kupokea Sh9.7 bilioni za kufadhili miradi ya maendeleo.
Mageuzi yaliyoanzishwa na Waziri Utumishi wa Umma na Vijana Margaret Kobia yalifutia kuzimwa kwa malipo ya madeni ya NYS ya kima cha Sh5.6 bilioni ya watu waliowasilisha bidhaa kwa shirika hilo miaka ya nyuma.
Alifanya hivyo, kutoa nafasi kwa ukaguzi wa kina wa namna kandarasi hizo zilitolewa.
Makandarasi au wakandarasi wa NYS walikaguliwa upya huku serikali ikijizatiti kuziba mianya yote iliyotumiwa kuiba pesa za umma.
Bajeti ya ziada iliwasilishwa bungeni, ili iidhinishwe, miezi miwili katika ya kumalizika kwa mwaka wa kifedha wa 2018/2019.
Duru kutoka Wizara ya Afya zilisema kuwa bajeti zote zilizofanyiwa mabadiliko zinahusu pesa ambazo tayari zimetumiwa. Kwa hivyo, wabunge watakuwa na nafasi finyu ya kukataa au kuifannyia mabadiliko bajeti hiyo.