MWANAMUME KAMILI: Ukware wa wanaume wa leo umechangia aibu mazishini!
Na DKT CHARLES OBENE
NIMEWAHI kuzungumzia haja ya wanaume wa leo kuwajibika kabla mauti na fedheha kuwafika siku za mwisho.
Hili liwe funzo kwenu wenye mazoea kuzaa na kuzalisha kiholela kisha kutoweka kama umande. Hivi majuzi palitokea kizungumkuti katika mazishi ya bwanyenye mmoja.
Hatuna budi kama wanaume kutathmini vipi tunavyoweza kuzuia fedheha katika shughuli ambazo ni muhali kuwepo aibu.
Haikujulikana walikotoka watoto watatu, watu wazima hasa waliodai kuzaliwa na mwendazake.
Walizuka tu kama mvua mazishini na kutaka kuona mwili wa “baba yao!” Wasabasi walinong’oneza kwamba wenda ndio watoto waliozaliwa mjini kisha mama yao akaondoka nao! Tangu “kuondoka kwa mama, hakuwajuza baba mzazi hadi kifo chake kilipotangazwa redioni.” Ndio mchezo wanaofanya kina yakhe wa leo.
Kwanza kabisa, vipi mwanamume anaweza kuzaa watoto na kuwaachia dunia kuwalea na kuwakuza hadi kifo chake?
Huu ndio mchezo ambao sharti tuusitishe! Hivi vita vya mazishini ni vita vya pesa na urathi! Ni vita vya kila mmoja kutaka kipande cha mali ya mfu.
Hivi sio vita vya mapenzi maana hakuna upendo usiojua mipaka ya mzaha. Ukware wa wanaume wa leo umechangia pakubwa kuwepo fedheha mazishini.
Punde tu kifo kinapomsibu mwanamume, huibuka majanga ya wanawake na pete vidoleni huku macho yamejaa huzuni licha ya nyuso zao kukosa haya! Yalikuwa wapi madege haya siku za jua? Iweje wanawake hawa kujificha kwa miaka na mikaka wakati mwanamume alikuwa mtu wa pumzi kisha kujitokeza ghafla kama upinde siku ya mazishi?
Hoja ni tofauti. Wengine tumetunga usaha kuwakebehi wanawake kufuata mikwanja wasiotolea jasho.
Sijui hilo la kutoleana jasho. Nijuavyo hasa ni kwamba paja lina gharama. Sharti lilipiwe kulikuza, kulikolezea mvuto, kulichezesha au hata kuligusagusa tu.
Wapo vilevile akina sisi tunaowasuta wanaume wasiotosheka na mke mmoja. Wenyewe walikwisha sema kwamba hawajamwona mja kala mara moja, tena chakula kimoja kikamshibisha kwa mwaka mmoja! Wanadai ni haki yao kula na kusaza.
Hekima ya wajinga haitolewi shuruti!
Ukweli ni kwamba mapenzi ya pesa yanakosha tena yanatisha mno!
Ole nyinyi vimwana mnaokaa vibarazani kuotea mafungu na mabunda ya wanaume.
Ole nyinyi mnaoharibu muda kujipodoa kwa kusudi la kumnasa na kumfurahisha mwanamume wa leo. Afadhali muda huo mngeutumia vyema viwandani au sokoni kuchuuza mboga na matunda.
Mtoto wa kike hana budi kukuza akili maana mwanamume wa leo si mwanamume kamili. Huu ndio wosia ninaowatunuku akina sisi tuliopotoka na dhana kwamba mwanamume yuko kwa masilahi ya mke. Mwanamume anaweza kukupa mara moja au mara mbili lakini kamwe haiwezi kuwa desturi!
Awali, akina sisi – yaani mimi na nyinyi limbukeni wa mapenzi – tuliteta kwa hamaki kwamba wanawake wa leo walikwisha janjaruka na wapo duniani kuchezesha kina yakhe mchezo wa pata potea potelea mbali. Hivyo ndivyo tulivyodhani! Ama kweli asiyenakili ya dunia hana akili! Nani bingwa zaidi ya mwanamume wa leo?
Hebu tuyaweke mambo wazi. Mwanamume wa leo ni mjanja upeo wa ujanja! Hakuna mke mjanja asiyeingia kiganjani ilmuradi mwanamume anadhamiria.
Hakuna mbinu za ufyonzaji na ukandamizaji wasizojua matapeli wanaume wa leo. Dhana kwamba wapo wanaume wakarimu tena walioradhi kumwaga pesa kwa masilahi ya mtoto wa mtu zimepitwa na wakati! Ndio maana wanawake wanasubiri hadi kifo angalau kutafuta haki!
‘Wanawake wajanja sana’
Sina haja kudunisha uwezo na ujanja wa wanawake katika dunia hii iliyojaa pwagu na pwaguzi.
Ila nitaweka wazi kwamba ngao ya mke ni kipochi chake! Afanye kazi zake. Ale na avae kwa nguvu zake. Lakini kamwe asiweke maanani kutegemea kitita cha mwanamume wa leo.
Baba na babu zetu wamekuwa shamba la nyikani. Kila hayawani na ndege wanaweza kulivamia wakalivuna kadri ya uwezo wao. Lakini mwisho wa siku, wataachika wameachama!
Mwanamume wa leo mchukie lakini heshimu mali yake. Hakuna mwanamume katika dunia zima anayeweza kumpa mke vya bure bila kumpangia mikakati jinsi mlaji atakavyolipia lije jua ije mvua. Nyie pwagu hamna chenu mbele ya pwaguzi waliokwisha jua mbinu zote kupata haki zao!
Na ibainike wazi kwamba penzi tamu halichuuzwi kitandani. Thamani yake haijui sarafu wala noti za mwanamume. Ole nyinyi wajanja mnaotumia singizio la mapenzi kuzoa ufadhili na masurufu ya wanaume. Mwanamue wa leo hana huruma wala soni na mtoto wa mtu aliyethubutu kula mali yake.
Mwanamume wa leo habembelezeki! Waweza kujitolea mhanga kumhonga mwanamume kwa shehena la mapenzi, tena mapenzi yaliyonogeshwa kitanga kama wanavyosema wenyewe lakini kama wewe ni wa kuachwa utaachika na kilio cha mbwa mdomo juu.
Mke anayekula vya mume mwishowe hujikuta pembeni hana chake hana wake! Ndio hawa wanaosubiri hadi kifo angalau kuleta macho ya huruma kama kweli huruma upo duniani.
Mume si mume kwa uwezo wa kuzalisha. Mwanamume huwa mwanamume kamili kwa jitihada ya malezi bora. Ole nyinyi mnaotafutwa mazishini!