• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kabras, KCB zaingia fainali ya Kenya Cup mwaka wa tatu mfululizo

Kabras, KCB zaingia fainali ya Kenya Cup mwaka wa tatu mfululizo

Na GEOFFREY ANENE

KWA msimu wa tatu mfululizo, fainali ya Lig Kuu ya raga nchini almaarufu Kenya Cup itakutanisha Kabras Sugar na KCB baada ya timu hizi kufagilia mbali Mwamba na Kenya Harlequin katika nusu-fainali mtawalia, Jumamosi.

Wanasukari wa Kabras, ambao wanashiriki fainali yao ya nne mfululizo, wamechapa Mwamba kwa alama 23-11 mjini Kakamega. Kipindi cha kwanza kilitamatika wakiwa juu 14-8. Kwa mara ya kwanza kabisa, fainali itaandaliwa katika ardhi ya Kabras, mjini Kakamega. Hii ni baada ya Kabras kumaliza msimu wa kawaida juu ya jedwali la ligi hii ya klabu 12.

KCB, ambayo inashiriki fainali yake ya tatu mfululizo, imeonyesha ukatili wake kwa kupepeta Kenya Harlequin 46-13 katika uwanja wake wa nyumbani mtaani Ruaraka jijini Nairobi.

Wanabenki wa KCB, ambao wamenufaika kudhalilisha Harlequin kupitia wachezaji wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Andrew Amonde na Jacob Ojee, hawajawahi kuchapwa na Kabras katika ligi. Walilemea Kabras 27-3 na kutwaa taji la mwaka 2015. Walitumia wembe uo huo kunyoa Kabras katika fainali za mwaka 2017 (36-8) na tena mwaka 2018 kwa alama 29-24. Kabras ilishinda ligi mwaka 2016 ilipopepeta Impala Saracens 22-5.

KCB ilikanyaga Kabras katika msimu wa kawaida msimu huu 44-20 kumaanisha bado wana kibarua kigumu kuvumbua mbinu ya kulipiza kisasi katika makala haya ya 49. 

You can share this post!

Afisi ya Rais yatengewa pesa ambazo ‘tayari...

‘Tangatanga’ wazidi kubanwa

adminleo