• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
JAMVI: Muthama afufua uhasama wake na Mutua kuhusu dai la ufisadi

JAMVI: Muthama afufua uhasama wake na Mutua kuhusu dai la ufisadi

Na BENSON MATHEKA

Uhasama wa kisiasa kati ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua na aliyekuwa seneta wa kaunti Johnson Muthama umezuka upya huku Muthama akifufua madai ya ufisadi dhidi ya serikali ya kaunti.

Kulingana na Bw Muthama, Dkt Mutua anafaa kukamatwa kwa kuhusika na ufisadi au aongoze wakazi kumkamata iwapo Tume ya Maadili na kupambana na Ufisadi (EACC) haitamkamata na kumfungulia mashtaka.

Mwanasiasa huyo alisema ana ushahidi kwamba Dkt Mutua amekuwa akitenga pesa kwa miradi ya maendeleo ambayo haitekelezwi. Ingawa anasisitiza kwamba yuko tayari kuwasilisha ushahidi alio nao kwa EACC na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Muthama hajaeleza unahusu nini.

Alipokuwa seneta kati ya 2013 na 2017, Bw Muthama aliwasilisha madai kwa EACC akimlaumu Dkt Mutua kwa kutofuata sheria kununua magari ya kutumiwa na mawaziri wa serikali yake. Mwaka jana, EACC ilisitisha kesi dhidi ya Gavana Mutua na kufunga faili ya uchunguzi.

Lakini Bw Muthama anasisitiza kwamba Dkt Mutua anahusika na ufisadi na kwamba ana ushahidi wa kutosha. Akiongea wiki jana katika kanisa la AIC Katwanyaa, Kaunti ya Machakos, Bw Muthama alimlaumu Dkt Mutua kwa kuendeleza ufisadi mkubwa akidai amekuwa akitumia miradi hewa kupora pesa.

Wadadisi wa siasa eneo la Ukambani wanasema kwamba nia ya Muthama ni kujiweka tayari kugombea ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 Dkt Mutua akimaliza kuhudumu kwa kipindi cha pili.

“Kuna tetesi kwamba Bw Muthama ana nia ya kugombea ugavana 2022 au amfadhili mtu kugombea kiti hicho na kwa kulaumu Dkt Mutua kwa ufisadi, anaandaa wakazi wa Machakos kwa kuwadhihirishia kwamba angali anatetea maslahi yao,” asema mdadisi Geff Kamwanah.

Anasema ikiwa ana ushahidi kwamba kuna ufisadi katika serikali ya kaunti ya Machakos unaomhusisha Dkt Mutua angeuwasilisha wa mashirika yanayofaa kwanza kabla ya kuropokwa kwenye mikutano ya hadhara.

Kulingana na Bw Kamwanah, Bw Muthama na wandani wake wanahisi kwamba Dkt Mutua amekula njama na seneta wa kaunti hiyo Bonface Kabaka ili wapore zaidi ya Sh346 milioni ambazo mahakama iliagiza Kabaka alipwe kwa kutoa huduma za kisheria kwa serikali ya kaunti.

“Nilimsikia mbunge wa Mavoko Makau akitilia shaka uamuzi wa mahakama iliyoagiza seneta Kabaka alipwe mamilioni ya pesa kwa kutoa huduma za kisheria kwa serikali ya kaunti. Sio sadfa kwamba Makau alitoa madai yake wakati mmoja Muthama alipotaka Dkt Mutua akamatwe,” alisema Bw Kamwanah.

Bw Makau anasema kwamba Bw Kabaka hafai kulipwa pesa hizo kwa sababu alikuwa mshauri wa masuala ya kisheria wa Dkt Mutua na alikuwa akilipwa mshahara.

Dkt Mutua amekuwa akidai kwamba wanaompiga vita ni watu wasiopenda maendeleo anayotekeleza chini ya kauli mbiu ya chama chake cha Maendeleo Chap Chap. Aliunda chama hicho baada ya kutofautiana na viongozi wa chama cha Wiper, akiwemo Muthama, muda mfupi baada ya uchaguzi mkuu wa 2013.

Bw Muthama alikataa kutetea kiti chake cha useneta kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 akisema hakutaka kufanya kazi na watu ambao wamekuwa wakipora mali ya wakazi wa Machakos.

Dkt Mutua amekuwa akilaumu viongozi wa Wiper kwa kufadhili madiwani wa chama hicho walio wengi katika bunge la kaunti kuhujumu ajenda yake ya maendeleo.

Anasema wapinzani wake hawafurahishwi na ushirikiano wake na mwenzake wa Kitui Charity Ngilu wa Kitui na mwenzake wa Makueni Kivutha Kibwana.

“Baadhi ya watu walishtuka nilipoungana na Profesa Kibwana na Charity Ngilu. Sasa wamebuni mbinu za kututenganisha lakini tunawaambia kwamba hawatafaulu. Jamii ya Wakamba inahitaji kuungana kupitia ajenda ya maendeleo,” alisema.

Kulingana na Bw Kamwanah, uhasama kati ya Muthama na Mutua zinatarajiwa kuongezeka vita vya ubabe wa kisiasa Ukambani zinavyoendelea kushika kasi.

“Kumbuka kwamba Muthama anamuunga kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuwa msemaji wa jamii ya Wakamba naye Mutua amekuwa akimezea mate wadhifa huo. Ikiwa wawili hao wataendelea kushikilia misimamo yao basi, hakuna wakati watapikwa kwenye chungu kimoja,” alisema Bw Kamwanah.

Mutua ambaye pia ana azma ya kugombea urais kama Kalonzo, amekuwa akiwataka wakazi kuwatema viongozi wenye umri mkubwa akiwalaumu kwa kupalilia umaskini kupitia siasa duni.

You can share this post!

JAMVI: Kauli ya Raila kuhusu SGR inamponza au inamjenga...

JAMVI: Ukosefu wa mrithi Mlima Kenya kunavyomfaidi Ruto

adminleo