• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Wakazi waishinikiza kaunti kukarabati barabara

Wakazi waishinikiza kaunti kukarabati barabara

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa mtaa wa Ngata katika Kaunti ya Nakuru wamelalamikia kuchoshwa na hali mbovu ya barabara ya Ngata-Roret msimu huu wa mvua.

Wakazi wanasema hata baada ya kutoa malalamishi kwa muda mrefu, hakuna hatua yoyote imechukuliwa.

Mashimo ya kina na mawe kandoya barabara yanaendelea kuwapa wanafunzi muda mgumu kwa kuhatarisha usalama wao.

Baadhi yao wanasema njia ni telezi, na wamelazimika kutumia njia mbadala kufika mjini, baada ya juhudi zao kushinikiza serikali ya kaunti kukarabati barabara hiyo, kuambulia patupu.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, Alfred Mwangi ambaye ni mwanabodaboda alilaumu Halmashauri ya Barabara za Mashinani (KeRRA) kwa kutowajibika kurekebisha barabara za mitaani.

Anasema KeRRA haijatilia maanani matumizi ya barabara za mashambani kwa sababu muda mrefu unachukuliwa kukagua barabara.

Alieleza kuwa wanasiasa wengi wamekuwa wakitumia,hali mbaya ya barabara hiyo kujipigia debe na pindi walipoingia mamlakani wakawasahau raia.

Wapita njia wa Roret-Ngata katika kaunti ya Nakuru hutatizika mno msimu wa mvua kwa barabara hii huwa haipitiki. Picha/ Richard Maosi

“Njia ya Roret Kuelekea Ngata ilipaswa kutengenezwa msimu wa kiangazi,mwaka uliopita,lakini cha kusikitisha ni pale mvua imeanza kunyesha,” alisema.

Mwaka uliopita wakazi wa Ngata walichanga 200,kila mmoja lakini hela hizo hazikutosha kuziba mashimo .

Kwa sababu ya gharama kubwa ya kununua mchanga wa kutengeneza njia,na kuandika vibarua wengi wao walikata tamaa na sasa wanasubiri serikali ya kaunti iwaokoe.

Ann Kibet anasema lazima KeRRA ichukue hatua ya kurekebisha njia, ili kuwezesha mazao ya shambani kufika sokoni kwa wakati.

Anasema kutokana na hali mbaya ya barabarani ndio sababu amekuwa akipata hasara kubwa tangia mazao yakiwa shambani hadi yanapovunwa.

Kunaponyesha, magari katika barabara hii hukwama. Picha/ Richard Maosi

Njia ya uchukuzi haipatikani na zile zinazopatikana sio salama kufikisha bidhaa kama mayai sokoni.

Mwakilishi wadi wa Ngata Daniel Mutahi anakubali kuwa hali ya barabara ni mbaya katika kaunti ya Nakuru hasa eneo la Roret.

Hata hivyo alieleza kuwa hajapokea hela zozote kutoka kwa serikali ya kaunti kurekebisha miundo mbinu duni ya njia.

“Tangu serikali ya ugatuzi iingie mamlakani, kaunti pekee ndiyo ilibakia na jukumu la kuhakikisha barabara zipo katika hali nzuri,” alisema.

Hata hivyo aliwahakikishia wakazi kuwa serikali ilikuwa na mipango ya kuwarekebishia barabara.

You can share this post!

JAMVI: Sababu kuu za pwani kulemewa kujibunia chama kimoja...

Chuo cha soka kinachonoa wanafunzi kuwa...

adminleo