• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Purukushani kiwanda cha Mchina kikifungwa sababu ya uchafu

Purukushani kiwanda cha Mchina kikifungwa sababu ya uchafu

Na LAWRENCE ONGARO

KIWANDA kimoja cha kutayarisha ngozi mjini Thika kimefungwa kutokana na mazingira machafu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Unyunyiziaji wa Maji na Chemchemi, Bw Joe Mutambo aliamuru kiwanda cha Times Unity, kifungwe mara moja.

Hata hivyo baada ya Bw Mutambo na ujumbe wake kufika katika kiwanda hicho, mmiliki wake wa asili ya Uchina alizua taharuki akitaka kukabiliana na polisi waliofika mahali hapo.

Alijaribu hata kumnyang’anya polisi bunduki jambo lililofanya maafisa wa polisi kumkabili haraka na kumweka pingu mikononi.

Ujumbe ulioandamana na Bw Mutambo uliachwa vinywa wazi kutokana na ujasiri wa Mchina huyo aliyejaribu kushika bunduki iliyokuwa na polisi.

Bw Mutambo na ujumbe wake walizuru viwanda kadha mjini Thika ambapo walishangaa kupata maeneo mengi kando ya viwanda hivyo bila sehemu za kumwaga maji taka baada ya kutengeneza bidhaa zao.

“Leo tumezuru kiwanda hiki cha Times Unity, na tumepata kuna makosa mengi yanayostahili kurekebishwa kabla ya kuwakubalia waendelee na kazi. Baadhi ya maswala muhimu tuliopata hayajafanyika vyema ni kukosa kibali cha kuendesha biashara hiyo, hawana barua yoyote, na maji yote yanayotoka katika kiwanda hiki yanasambaa katika mto Chania huku wananchi wengi wakiyatumia maji hayo,” alisema Bw Mutambo.

You can share this post!

Chuo cha soka kinachonoa wanafunzi kuwa...

Man City watwaa ufalme wa EPL kwa mara ya pili mfululizo

adminleo