• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Man City watwaa ufalme wa EPL kwa mara ya pili mfululizo

Man City watwaa ufalme wa EPL kwa mara ya pili mfululizo

NA MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

MANCHESTER City waliweka historia katika soka ya Uingereza Jumapili kwa kunyanyua ubingwa wa taji la EPL kwa mara ya pili mfululizo.

Ushindi wa 4-1 uliosajiliwa na Man-City dhidi ya Brighton hapo jana uwanjani American Express Community uliwawezesha kuwapiga kumbo Liverpool ambao wamekuwa wapinzani wao wakuu katika kampeni za msimu huu.

Mvamizi Sergio Aguero aliwafungulia Man-City ukurasa wa mabao kunako dakika ya 28, sekunde chache baada ya Glenn Murray kuwapa Brighton bao la kwanza.

Licha ya kuwabamiza Wolves uwanjani Anfield, Liverpool ya kocha Jurgen Klopp ilisalia katika nafasi ya pili kwa alama 97, moja nyuma ya Man-City.

Kabla ya kuwaongoza masogora wake kuvaana na Brighton hapo jana, kocha Pep Guardiola alikiri kwamba ufanisi wa kunyanyua ufalme wa taji la EPL kwa msimu wa pili mfululizo ni hatua kubwa zaidi katika makuzi ya kikosi chake.

Isitoshe, aliwapa mashabiki wa Man-City uhakika wa kusalia uwanjani Etihad licha ya kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua kambini mwa Juventus.

Guardiola, 48, amekuwa akihemewa pakubwa na Juventus ambao kwa sasa wanatarajiwa kuanza kuwinda maarifa ya Mauricio Pochettino wa Tottenham Hotspur kwa nia ya kulijaza pengo la Allegri.

Kwa mujibu wa Guardiola, kubwa zaidi katika malengo yake kwa sasa ni kuhudumu kambini mwa Man-City kwa misimu miwili zaidi kwa matarajio ya kuwanyanyulia waajiri wake taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kufikia 2021.

“Guardiola yuko radhi kurefusha mkataba wake ugani Etihad kwa kipindi cha miaka miwili zaidi kwa nia ya kutia kapuni taji la UEFA ambalo linastahiwa pakubwa na mmiliki wa Man-City, Sheikh Mansour.

Mchuano wa jana ulikuwa wa mwisho kwa nahodha Bruno Saltor kuwachezea Brighton kabla ya kustaafu mwishoni mwa msimu huu.

Man-City walijibwaga ugani kwa kipute hicho wakilenga kutia kapuni alama tatu ili kuhifadhi ufalme wa Ligi Kuu ya EPL na hivyo kuwapiga kumbo Liverpool ambao wamekuwa wakuwa wapinzani wao wakuu muhula huu.

Bao la nahodha Vincent Kompany dhidi ya Leicester City katika mechi ya iliyowakutanisha uwanjani Etihad mwanzoni mwa wiki jana lilidhihirisha ukubwa wa uwezo wa Man-City katika kivumbi cha EPL msimu huu.

Baada ya kutia kapuni jumla ya alama 100 msimu jana, Man-City walijizolea pointi 98 katika kampeni za muhula huu. Ufanisi huo una maana kwamba Man-City wamekuwa wakitia kapuni angalau alama 2.6 kutokana na kila mchuano kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita.

Liverpool walioandamwa na mkosi kwa mara nyingine, kwa sasa wanapigiwa upatu wa kutia kibindoni ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Man-City ambao wamesajili ushindi mara 32, kuambulia sare mara mbili na kushindwa mara nne wamepoteza jumla ya alama 16 kufikia sasa huku Liverpool wakipigwa mara moja pekee katika mechi iliyowakutanisha na Man-City uwanjani Etihad mwanzoni mwa Januari 2019.

“Ni fahari na tija tele kufikia hapa tulipo kwa sasa. Kampeni za msimu huu hazijakuwa rahisi kwa kikosi chochote. Ni muujiza kuona Man-City wakitawazwa mabingwa, hasa ikizingatiwa kwamba Liverpool waliwahi kujivunia pengo la alama saba kileleni mwa jedwali hadi kufikia Disemba 2018.

Chelsea ambao tayari wamefuzu kwa kipute cha UEFA msimu ujao, walikuwa wageni wa Leicester uwanjani King Power. Kikosi hicho cha kocha Maurizio Sarri hata hivyo kilihitaji kusajili ushindi ili kujipa hamasa ya kujitahidi vilivyo dhidi ya Arsenal katika fainali ya Europa League mnamo Mei 29 jijini Baku, Azerbaijan. Arsenal watafuzu kwa kampeni za UEFA msimu ujao iwapo watashinda Chelsea.

Tottenham ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini walikuwa wenyeji wa Everton. Chelsea wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 74, nne zaidi kuliko Arsenal ambao wanaorodheshwa mbele ya Manchester United wanaokamata nafasi ya sita chini ya mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer.

Akihojiwa na wanahabari kabla ya Man-City kuchuana na Brighton, Guardiola alikiri kwamba ukubwa wa viwango vya ushindani katika kampeni za EPL msimu huu ulichangia mshindi wa EPL kuamuliwa katika siku ya mwisho.

Kwa upande wake, Guardiola alisema Liverpool wanajivunia kikosi imara kilicho na uwezo wa kutwaa ubingwa wa UEFA msimu huu. Aidha, alikiri kwamba uwepo wa Sadio Mane, Robert Firmino na Mohamed Salah kambini mwa Klopp ni sifa inayofanya Liverpool kuwa miongoni mwa klabu zenye safu bora zaidi za uvamizi katika ulimwengu wa soka.

“Wana kikosi imara ambacho kilijisuka vilivyo katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji. Wanajivunia uthabiti katika takriban kila idara. Hii ni sifa ya kikosi ambacho kinatawaliwa na kiu ya kunyanyua mataji ya haiba kubwa,” akasema Guardiola kwa kudokeza uwezekano wa Man-City kujitoma sokoni mnamo Januari 2019 na kusajili mabeki wa viwango vya juu zaidi.

“Ukitaka kutwaa mataji katika kampeni zozote, ni lazima usajili matokeo mazuri. Bila shaka Liverpool na Man-City wamedhihirisha kwamba wana huo uwezo katika soka ya Uingereza na bara Ulaya msimu huu,” akaongeza.

Katika misimu minane kati ya 10 iliyopita, klabu ambayo imekuwa ikiongoza jedwali la EPL baada ya kupigwa kwa nusu ya michuano yote kufikia wakati wa Krismasi imekuwa ikitwaa ubingwa. Hata hivyo, Liverpool iliwahi kuongoza mara mbili kufikia wakati kama huo mnamo 2008-09 na 2013-14 kabla ya kupitwa na kuambulia nafasi ya pili mwishowe baada ya kuzidiwa maarifa na Man-United na Man-City mtawalia.

Hili ni jambo ambalo Klopp ameshindwa pia kulirekebisha muhula huu kambini mwa Liverpool ambao walipoteza mchuano mmoja pekee kati ya 38 katika EPL msimu huu.

MATOKEO YA EPL

Tottenham 2-2 Everton

Man-United 0-2 Cardiff City

Watford 1-4 West Ham United

Southampton 1-1 Huddersfield

Leicester City 0-0 Chelsea

Fulham 0-4 Newcastle Utd

Liverpool 2-0 Wolves

Palace 5-3 Bournemouth

Brighton 1-4 Man-City

Burnley 1-2 Arsenal

You can share this post!

Purukushani kiwanda cha Mchina kikifungwa sababu ya uchafu

HISTORIA: Liverpool timu ya kwanza kuzoa pointi zaidi ya 90...

adminleo