Wakenya wadaka mkwanja mbio za Lagos Marathon
Na GEOFFREY ANENE
WAKENYA Ronny Kiboss, Benjamin Bitok na Rodah Jepkorir walijishindia Sh4 milioni, Sh3 milioni na Sh403, 986 baada ya kumaliza mbio za Lagos Marathon katika nafasi za pili, tatu na tisa nchini Nigeria, Februari 10, 2018, mtawalia.
Mfaransa Abraham Kiprotich, ambaye ni mzawa wa Kenya, alinyakua taji la wanaume kwa saa 2:15:02 na kutia kibindoni Sh5 milioni.
Kiboss, ambaye pia alimaliza makala ya mwaka 2017 katika nafasi ya pili, alijaribu mbinu zote kutwaa ubingwa, lakini akazidiwa maarifa na Kiprotich katika mita 600 za mwisho.
Muda wa Kiprotich ni rekodi mpya ya Lagos Marathon. Alifuta sekunde moja kutoka kwa rekodi ya mkimbiaji aliyewahi kutimka kasi ya juu kabisa katika ardhi ya Nigeria ya saa 2:15:03 iliyowekwa na raia wa Jamhuri ya Ireland, Sean Healy mwaka 1971. Kiboss na Bitok walikamilisha umbali huo kwa saa 2:15:24 na 2:15:27, mtawalia.
Waethiopia Almenesh Herpha (2:38:23), Tigist Girma (2:38:34) na Ayelu Abele Hordofa (2:38:39) walifagia nafasi tatu za kwanza katika kitengo cha wanawake.
Jepkorir, ambaye alikuwa akitetea taji la kitengo cha wanawake, anashikilia rekodi ya Lagos Marathon ya wanawake ya saa 2:37:52 aliyoweka mwaka 2017.