Makala

TAHARIRI: Twahitaji mjadala wa visa vya mauaji

May 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

VISA vya watu kuuana au kujiau vimazidi kuwa gumzo lii hapa nchini.

Jumapili kuliripotiwa visa kadhaa, ambapo katika kaunti ya Trans Nzoia mwanamke alimuua mke mwenza, huku katika kambi ya jeshi la Wanamaji ya Likoni, Mombasa, mwanajeshi aliyekua likizoni alienda kazini tu kwa lengo la kumuua afisa mwenzake na kisha akajimaliza.

Katika kisa cha kaunti ya Trans Nzoia, polisi wanamzuilia mwanamke anayedaiwa kumwotea mke mwenza mwenye mtoto mchanga akiwa anaoga bafu, akamshambulia na kumuua.

Ni juzi tu ambapo mwanamke mwengine katika kaunti ya Meru inadaiwa alimkata kwa panga mwanamke aliyemdhania alikuwa akishiriki mapenzi ya pembeni na mumewe.

Hii ni sehemu tu ya msururu wa matukio ambapo watu katika maeneo mbalimbali ya nchi wamekuwa wakiua wenzao au kujitoa uhai kwa sababu ndogo ndogo ambazo, kama kungekuwa na mpangilio maalum wa kuzifuatilia, vifo hivyo vingeepukika.

Kila kukicha kunaripotiwa visa vya hata watoto wadogo kujinyonga au kuwaua watoto wenzao.

Hali hii inadhihirisha kuwepo kwa shida ambayo hakuna mtu anayeonekana kujali kuitambua na kuitatua.

Viongozi wa dini wanaonekana kuhubiri zaidi kuhusu pesa kuliko kuwaelimisha waumini kuhusu kuvumiliana, kuzikabili shida kiume na nafasi ya uhai katika mfumo mzima wa maisha.

Katika makanisa, maskofu wakuu wangekuwa sasa hivi wanatengeza mada maalum za kueleza kwa nini Mwenyezi Mungu aliumba wanadamu na ni yeye anayestahili kuchukua uhai wa mtu.

Waislamu vile vile, wanazingatia zaidi kuzungumzia mema ya mtu binafsi na nafasi ya kuingia peponi kwa kusali, kufunga au kutoa zaka. Ni nafasi kidogo sana inayotengwa kuwaelimisha waumini kuwa, kuua ni dhambi kubwa.

Serikali imekuwa ikiandaa maombi ya kila mwaka, zaidi yakisemekana kuwa ya kuombea amani. Kwa hali ilivyo sasa, nchi hii inahitaji zaidi mjadala wa kuhusu mambo yanayowasukuma watu kujiua au kuua wengine.

Waziri anayehusika na mambo ya Ndani, Dkt Fred Matiang’i anapaswa kuitisha kikao cha dharura na washauri nasaha, madaktari wa akili, viongozi wa kidini na wadau wengine, kutambua sababu zinazofanya watu wasithamini maisha.