Makala

WAKILISHA: 'Gavana' mwenye umri mdogo zaidi

May 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA umri wa miaka 19 pekee anawakilisha vijana katika Kaunti ya Bomet, wadhifa alioupata mwaka 2018 akiwa na umri wa miaka 18 pekee.

Kutana na Abby Chebet, Gavana wa Vijana wa Kaunti ya Bomet na mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Multimedia University of Kenya.

Kama Gavana wa vijana, jukumu lake kuu ni kuratibu shughuli za kuwahami vijana kwa elimu na kuhakikisha kwamba wanashirikishwa katika utekelezaji wa sera za vijana katika kaunti ya Bomet.

Bi Chebet aliteuliwa katika wadhifa huu Novemba 2018 huku akiwabwaga wapinzani wanne ambapo anatarajiwa kuhudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kuteuliwa kwake kulitokana na mchango wake katika jamii kupitia wakfu alioanzisha wa The Lady’s Heart Foundation.

Kupitia mradi huu Bi Chebet amejitwika jukumu la kuwapa wasichana katika maeneo ya mashambani nguvu kielimu na katika masuala ya usafi wa mwili.

Mafunzo haya yanahusisha umuhimu wa kukumbatia elimu kama ala ya kuangamiza visa vya mimba za mapema.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, tumeandaa vikao vya unasihi kupitia shule, makanisa na mabaraza ya machifu katika maeneo ya mashambani ambapo tumefikia zaidi ya wasichana 50,” aeleza.

Katika jitihada hizi pia ameunganisha wanafunzi kadha wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakisaidia katika shughuli hizi. “Kufikia sasa kikundi hiki kina wanachama wanaojumuisha wanafunzi 85 kutoka vyuo vikuu mbalimbali,” aeleza.

Pia, wamekuwa wakiwafunza wasichana kuhusu usafi wa mwili hasa wakati wa hedhi. “Katika harakati hizi sisi hutoa msaada wa visodo, bali na kusaidia wanafunzi kutoka familia maskini kulipa karo,” asema.

Wakfu wawafaa wakazi

Aidha, wakfu huu umekuwa ukisaidia wakazi wa kijiji cha Chemengwa, eneo la Bomet, kupata mahitaji muhimu kama vile vyakula, mavazi na hata vifaa vya masomo kama vile vitabu.

“Tumekuwa tukifanya hivi kwa kuungana na wahisani ambao baada ya kutoa misaada, jukumu letu linakuwa kuwatambua wakazi wanaohitaji usaidizi zaidi,” aeleza.

Ni shughuli ambazo zimewapeleka katika shule mbalimbali za msingi na za upili katika jitihada hizi, ambapo wametembelea Kaunti za Bomet, Kericho, Nakuru, Nandi, Nyeri, Kajiado na Narok.

Na tayari jitihada zao zimeendelea kuzaa matunda.

“Kwa mfano kumekuwa na ongezeko la idadi ya wasichana wanaojiunga na shule ya upili. Aidha, wasichana wengi katika maeneo ambayo tumetembelea, sasa wanaelewa kuhusu masuala ya hedhi,” aeleza.

Ni safari iliyoanza Desemba 2017 huku visa vya wasichana kushika mimba vikichangia uamuzi wake kuingilia kati.

“Nilipokuwa mdogo, nilishuhudia wasichana wengi wakiacha shule kwa sababu ya kushika mimba, na hivyo nilijua kwamba hili ni tatizo ambalo ningetaka kulishughulikia mara moja nikipata nafasi,” aeleza.

Mwisho wa mwezi huu Aprili 2019 wamepanga kampeni kubwa.

Hafla hii imepangiwa kufanyika Mei 28 ambapo kwa ushirikiano na muungano wa kitaifa wa wanafunzi wa udaktari (SCORA), watakuwa na kampeni nchini kote.

“Kauli mbiu yetu itakuwa ‘End Period Poverty’ ambapo wanachama wetu watatembelea wasichana katika shule za msingi, mitaani au katika vitongoji duni, katika makao ya kuokoa wasichana na hata wale walio magerezani ambapo tunapanga kuendesha mafunzo ya usafi wa mwili wakati wa hedhi.

Pia, tunapanga kutoa misaada ya visodo, vile vile kutoa huduma za kimatibabu,” aeleza.

Shughuli hii inatarajiwa kufanyika katika kaunti mbalimbali ikiwa ni pamoja na Nairobi, Kiambu, Nakuru, Eldoret, Kisumu, Kajiado na Bomet.