Makala

AUNTY POLLY…: Nina hofu kujiunga na Chuo Kikuu

May 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

MWAKA 2020 natarajiwa kujiunga na chuo kikuu. Hata hivyo mimi ni mwoga sana na nimeanza kuingiwa na hofu ya kukutana na watu wapya wakati huo utakapotimia. Nifanyeje kupunguza hisia hizi?

Benta, 19, Nairobi

Ni vyema kwamba umejitokeza kuzungumzia suala hili. Ningependa kukuambia kwamba mojawapo ya njia mwafaka za kukabiliana na hisia hizi ni kuwazia nini hasa kinachokutia hofu ya kukutana na watu wapya. Ikiwa unashindwa ni vipi utakavyowasiliana na wanafunzi wapya utakaokutana nao ifikipo mwaka ujao, jambo la busara ni kufanya mazoezi. Jizoeshe ukiwa peke yako jinsi ya kujitambulisha kwa watu unaokutana nao kwa mara ya kwanza. Mbali na hayo, jipe ujasiri zaidi kwa kukutana na watu wapya. Waweza afikia hili kwa kuanza kuhudhuria mikutano ya kijamii, kidini, au kwa kutembelea maeneo ya burudani kujipa mazoea zaidi.

 

Mimi ni msichana wa kidato cha tatu na wazazi wangu hawana habari kuwa nina mpenzi. Mpenzi wangu ana umri wa miaka 17. Nina hofu ya kuwaambia kwa sababu wamekuwa wakinisisitizia kwamba sipaswi kujiingiza katika uhusiano ya kimapenzi kabla ya ndoa. Hata hivyo nimeshiriki tendo la mahaba na huyu kijana mara moja na sasa nina hofu kuwa huenda ameniambukiza maradhi ya zinaa. Sijui nifanyeje kupata matibabu pasipo wazazi wangu kujua kwani sina hela na njia ya kipekee ya kufanya hivyo ni kupitia bima ya afya ya babangu. Naomba ushauri?

Caroline, 17, Mombasa

Suala la kwanza ningependa kukuambia ni kwamba kiumri ungali mdogo kuanza kujihusisha na mambo haya. Aidha, ningependa kukusisitizia kwamba wewe mwenyewe unapaswa kuwajibikia usalama wako kiafya. Unapaswa kujua kwamba ni hatari kushiriki tendo hilo bila kinga hasa ikiwa unashiriki na mtu usiyemuamini. Wasiwasi ulio nao ni ishara tosha kwamba humuamini mvulana huyu. Itakubidi kuwajibika na kuzingatia suala la afya yako na hiyo inamaanisha kujikinga kutokana na maradhi ya zinaa vilevile mimba zisizotarajiwa. Kuhusu suala la matibabu, kuna vituo vya afya kote nchini vinavyotoa huduma ya masuala ya uzazi bila malipo ambapo waweza kutembelea.