Habari

Tulizika vidoli kuwazima waliotaka kunyakua ardhi yetu, wanandoa wafunguka kortini

May 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

GEORGE ODIWUOR na CHARLES WASONGA

WANANDOA katika Kaunti ya Homa Bay ambao walizika vidoli viwili wakidai ni mapacha wao Jumanne waliambia mahakama walitenda kitendo hicho cha ajabu ili kuwazuia watu fulani kunyakua ardhi yao.

Bi Beryl Akinyi na mumewe Benson Onyango walimwambia Hakimu Mkazi wa Mbita Japheth Bii kwamba walitaka kukinga ardhi yao ambayo wastawishaji fulani walikuwa wakitaka kunyakua.

Wawili hao walilenga kuacha alama za makaburi katika ardhi hiyo ili kuwaogofya wanyakuzi. Miongoni mwa jamii ya Waluo, ardhi yenye makaburi huwa sio rahisi kunyakuliwa.

Uwepo wa makaburi pia huwa ithibati ya umiliki wa ardhi ambayo haina hatimiliki.

Wandoa hao walitumia imani hii na kujifanya kujaliwa watoto pacha ambao hatimaye walifariki na wakazikwa katika ardhi hiyo.

Bi Akinyi aliwahadaa majirani na jamaa zake kwamba aliwapoteza watoto hao wawili licha ya kusaka huduma za matibabu kutoka katika hospitali tatu; Hospitali ya Rufaa ya Homa Bay, Hospitali ya Aga Khan iliyoko mjini Kisumu na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Nairobi.

Hata hivyo, iliibuka kwamba habari hizo hazikuwa kweli Jumanne.

Njama ya wanandoa hao ilifichuliwa pale wakazi walipotaka kujua ni kwa nini waliwazika “watoto” wao bila kuruhusu mtu yeyote kutizama maiti yao, jambo ambalo mi kinyume na tamaduni za Waluo.

Hapo ndipo wakazi hao wa kijiji cha Kamsama, katika eneobunge la Suba Kaskazini waliwashambulia wakitaka kujua ukweli kuhusu mimba ya Bi Akinyi.

Ukaguzi wa kimatibabu uliofanya katika Kituo cha Utafiti kuhusu Wadudu (ICIPE) mjini Mbita ulibaini kuwa mama huyo hakuwa amejifungua hivi karibuni.

Lakini Bw Onyango alisisitiza mbele ya maafisa wa polisi kwamba mkewe amekuwa akibeba ujauzito.

Hata hivyo, Jumanne wawili hao walibadili kauli yao walipofunguliwa mashtaka kortini.

Wanandoa hao walishtakiwa kwa kutoa habari za uwongo kwa polisi kinyume na sheria.

Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Mei 7, 2019, Bw Onyango na Bi Akinyi walitoa habari za uwongo kwa Inspekta Mkuu Joseph Kutere na Konstebo Christopher Ndegwa kwamba mama huyo alijifungua watoto mapacha waliofariki katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.

Wakiri makosa wakisema walitoa habari za uwongo kwa lengo la kukinga kipande cha ardhi ambacho mtu fulani alipania kunyakua.

Japo waliomba wasamehewe, hakimu aliwatoza faini ya Sh50,000 la sivyo wafungwe gerezani kwa miezi sita.

Hakimu Bii aliamuru wazuiliwe rumande katika gereza la Homa Bay hadi watakapolipa faini hiyo.