Magoha na Sossion kujadiliana kuhusu mtaala mpya
Na VITALIS KIMUTAI
CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kitakutana na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kuhusu masuala tata ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu, katika kile maafisa wake wanasema yatakuwa mazungumzo ya kubaini mbivu na mbichi.
Katibu Mkuu wa Knut Bw Wilson Sossion alisema Jumanne asubuhi kuwa mkutano huo ulipangiwa kufanyika saa tisa alasiri katika makao makuu ya chama hicho.
“Tutakutana na Prof Magoha baadaye alasiri na kumwambia waziwazi kwamba mtaala mpya wa Competency Based Curriculum (CBC) ulisambaratika kabla haujaanza.
“Vilevile, barua zilizotumwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuwasimamisha kazi kwa muda walimu 160 ziondolewe. Nazo sera zenye mapendeleo zinazotekelezwa na wizara pasipo uungwaji mkono kisheria, zisitishwe,” Bw Sossion aliambia Taifa Leo kwa simu.
Aliongeza: “Wizara ya Elimu inawalazimishia walimu sera zisizo na msingi wowote katika sheria, na wanapoibua maswali wanatishiwa kufutwa kazi ama kusimamishwa kwa muda, na mara nyingi wanatumiwa polisi.”
“Huwezi kutumia nguvu za kimabavu kuendesha sekta ya elimu, na kutuma polisi kuwahangaisha walimu wanapoibua masuala tata ya kikatiba. Hii sio nchi inayotawalwa na polisi na walimu lazima waheshimiwe. Hata polisi walifunzwa na hao walimu wanaowadhulumu.”
Prof Magoha alisema hapo awali kwamba hana mamlaka yakuwarejesha kazini walimu waliosimamishwa kazi kwani ni jukumu la TSC, ambalo ni tume huru, hoja inayotarajiwa kuibua mjadala mkali kwenye mkutano na Knut.
Wizara ya Elimu inatoa mafunzo kwa walimu 68,490 wanaofunza darasa la kwanza hadi nne kwenye mtaala mpya, na walimu wakuu 22,830 kote nchini.
Wakati huohuo, Bw Sossion alisema kuwa katika mchakato wa marekebisho ya Katiba walimu watapendekeza kupunguzwa kabisa kwa mamlaka ya TSC kama tume huru na kuigeuza kuwa idara chini ya Wizara ya Elimu.
“TSC imefeli kabisa kutekeleza jukumu lake na inawatesa walimu badala ya kushughulikia maslahi yake,” alieleza katibu mkuu huyo.
Knut imekuwa katika mvutano na TSC kwa miaka mingi kuhusu walimu kupandishwa vyeo, kuajiriwa na mishahara.