Amri wanaume waoe wake 2 au wakamatwe ni habari feki – Mswati
MASHIRIKA Na CHARLES WASONGA
SERIKALI ya Eswatini Jumanne ilikana habari zilizosambaa mitandaoni kwamba Mfalme Mswati III, ameamuru wanaume wote nchini humo kuoa angalau wake wawili kila mmoja la sivyo wasukumwe gerezani.
Kulingana na habari hizo zilizochapishwa katika tovuti ya gazeti la Zambia Observer, amri hiyo ilipaswa kuanza kutekelezwa mwezi wa Juni. Dakika chache baadaye, habari hizo feki zilisambazwa katika tovuti nyingine za habari.
Mfalme Mswati ambaye ana wake 14 na zaidi ya watoto 25 anafahamika kama kiongozi ambaye huishi kwa anasa ilhali asilimia 63 ya wananchi 1.3 milioni katika ufalme wake wanazongwa na umaskini wa kiwango cha juu.
Habari hiyo iliyochapishwa Jumatatu inasema kuwa “serikali itafadhili ndoa za wanaume ambao watatii amri ya Mfalme na kuoa wanawake wawili na zaidi.” Utawala huo pia ulitangaza kuwajengea wanaume hao nyumba za kuishi na wake zao.
Lakini Jumanne, msemaji wa Serikali Percy Simalane alikana habari hizo akizitaja kama za uwongo na ambazo zinalenga “kumharibia sifa kiongozi wetu na kuwa kuharibu uhusiano wake na raia.”
“Mfalme hajaotoa tangazo kama hilo na kwani suala hilo halijawahi kuibuliwa katika Kasri na mtu yeyote,” akasema Bw Simalane.
Alisema taarifa hiyo ililenga kudharau na kudunisha ufalme na tamaduni za Eswatini. “Hiki ni kielelezi cha uanahabari ambao umepotoka kimaadili,” akaongeza.
Serikali imeitaka gazeti hilo kuondoa habari hiyo na kuomba msahama kwa Mfalme Mswati III.