• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
NDIVYO SIVYO: Kufa na kufariki hutofautiana kimaana na hutegemea miktadha ya matumizi

NDIVYO SIVYO: Kufa na kufariki hutofautiana kimaana na hutegemea miktadha ya matumizi

Na ENOCK NYARIKI

MUKTADHA una namna fulani ya kuelekeza matumizi ya maneno.

Kuna baadhi ya maneno ambayo ingawa maana ya msingi huelekea kufanana, miktadha ya matumizi huibua tofauti baina ya maneno yenyewe.

Mfano mzuri wa maneno hayo ni “kufa” na “kufariki” ambayo tutayaangazia katika makala haya.

Huenda maana ya msingi ya maneno mawili tuliyoyataja isitusaidie katika kuyatofautisha kwa sababu yanakurubiana sana hivi kwamba neno moja linachukuliwa kuwa kisawe cha jingine.

Kwa upande mwingine, jamii hupendelea kulitumia neno fariki wakati wa kuzungumzia au kueneza habari za tanzia.

Si kwamba neno kufa haliwezi kutumiwa kwa namna hiyo ila makubaliano baina ya wanajamii ni kuwa neno fariki limebeba dhana ya upole kuliko ‘kufa’ hivyo basi hutumiwa kuisanifisha na kuisarifu lugha.

Hata hivyo, neno “fariki” haliwezi kutumiwa, kwa mfano, kuelezea kifo cha mnyama.

Anayelitumia neno hilo kwa namna hiyo huchukuliwa na jamii kuwa hajui kuisarifu lugha.

Maneno, kufariki, kuaga dunia, kutupa mkono na ujauzito hutumiwa kueneza sifa ya binadamu.

Nilipomwuliza Profesa Wamitila iwapo kunayo maana nyingine inayoweza kuhusishwa na neno ‘kufa’ na inayolitofautisha na ‘kufariki’ katika msemo “Heri kufa kuliko kufariki’’ hivi ndivyo alinijibu:

“Ipo ndiyo; ukiangalia katika matumizi ya kila siku kama vile kufa ganzi, neno hilo liko katika ngazi ya afadhali zaidi kuliko kufariki ambako kuna fahiwa ya kujitenga kabisa pasi na uwezekano wa kurejea katika hali ya awali(inavyoweza kutokea baada ya kufaliji au kufa ganzi). Maneno hutofautiana katika fahiwa zake…ndiyo maana huwa tunasema hakuna visawe mia fil mia!’’

Waama, huenda tusiione tofauti baina ya maneno “kufa” na “kufariki” hadi tutakapoiondoa kabisa katika mawazo yetu maana ya msingi ya maneno yenyewe (ile ya kuondokewa na uhai) na kuona matumizi yake kijazanda na jinsi mbinu hiyo inavyoibua tofauti ya kimaana baina ya maneno yenyewe.

Kwa mintarafu hii, neno “kufa” limebeba maana ya kuwa katika hali ya kuweza kurekebishika ilhali kufariki ni kinyume chake.

Licha msemo tulioutaja, neno kufa hutumiwa katika semi tofauti likiwa na maana tofauti. Kwa mfano, katika msemo “Sikio la kufa halisikii dawa’’, haiyumkiniki kwamba neno hilo linaleta fahiwa ya kukata roho ila linaibua dhana ya ukaidi. Ndivyo ilivyo katika semi ‘kufa kuzikana’ ambapo maana inayoibuliwa ni ile ya urafiki wa dhati.

Alhasili, tofauti za maneno hujitokeza wazi zaidi yanapoangaliwa nje ya maana ya msingi.

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Kiswahili kitafana iwapo wanahabari...

VITUKO: Ndoto yamchochea Sofia kuyoyomea mtaani Ngomeni...

adminleo