Makala

Biashara ya njugu karanga na korosho ina faida

May 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

HUKU vijana wengi hapa nchini wakilia kuwa hakuna nafasi za kazi katika uchumi, kuwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inaonekana wazi kupendelea wazee katika nafasi zilizopo, uamuzi ni wa mtu binafsi; aendelee kulalamika na kulialia au atumie bongo lake ajinusuru.

Leo hii kijana Walter Kamau anakufichulia kuwa kuna biashara ya pesa za haraka na ambayo bora tu uwe unapenda mapishi, utajipa afueni kuu na utajiri.

“Kuja nikuelimishe jinsi ya kukaanga njugu na korosho kisha uingie mtaani na uanze kutumia ulimi wako kusaka wateja na hatimaye utarudi hapa ukinipa shukrani zako kwa kukusaidia,” anasema Kamau.

Bw Kamau ambaye ni mlemavu anasema kuwa hakutozi ada yoyote kukupa maarifa haya, bora tu ukinufaika na ujipe uthabiti wa pato, basi roho yake itatulia kwa raha akijua kuwa amechangia kumpa binadamu mwenzake mbinu ya kujiendeleza.

Walter Kamau katika afisi zake za kukaanga na kupakia njugu karanga na korosho katika mtaa wa Zimmerman, kaunti ya Nairobi. Picha/ Mwangi Muiruri

Anakuambia kuwa hesabu ndani ya biashara hii haihitaji Kizungu kingi au Kiswahili kingi kuelezeka kwa urahisi, “bali chukua kalamu na karatasi ujue kuwa kwa kila Sh10 utawekeza katika biashara hii, pato lako litakuwa Sh30.”

Anasema kuwa hilo lina maana kuwa mtaji wa Sh10 unakupa faida ya Sh20.

Anakuelezea kuwa kupata hizi njugu karanga na korosho sio suala la ufumbuzi, bali ni kuingia sokoni na kujinunulia kipimo chako cha ukadiriaji wa uwezo wako kimtaji.

“Unaweza ukanunua kwa kipimo cha kilo tano, 10 au hata zaidi. Bora tu ujue kuwa kiwango unachonuia kuzindua nacho biashara hii kinakutosha,” anasema.

Anasema kuwa utahitaji jiko, sufuria na moto pamoja na chumvi.

“Kuna wengine watakuambia usake mafuta ya kukaanga… Kwa kuwa ladha ya njugu na korosho mitaani huwa ya aina ya kukaushwa na ya kukaangwa. Bora tu uzingatie viwango vya joto, usije ukaunguza njugu zako au korosho. Na ukiamua kuzikaanga, usiweke mafuta mengi ya kulowesha. Fanya kila kitu kwa utaratibu,” anahimiza.

Anakuambia kuwa suala hili sio la kuelimishwa kwa karo au uchukue muda mwingi katika skuli ukisaka shahada. La!

“Ili kuelewa kinachohitajika, kwanza saka mchuuzi wa njugu karanga sokoni. Jinunulie sampuli kama mteja. Agiza za kukaangwa, agiza za kukaushwa na hatimaye hata ukipenda, uliza huyo anayekuuzia maswali ya ni wapi unaweza ukajinunulia za kuzindua biashara yako,” anasema.

Uteja wa wazi

Anasema kuwa uteja wa bidhaa hizi ni wa wazi.

“Bora tu ujue kuweka ile mitego ya kuwindana na fuko na panya… Usifuate wachuuzi wengine ambao wanauza bidhaa hizi. Kuwa mjanja, fuata wateja wako katika mahali waliko, kuwa chapuchapu na uwe na ulimi wa kuvutia wateja. Lenga watafunaji Miraa na Muguka; hao ndio wateja thabiti wa njugu na korosho,” anasema.

Anakuambia kuwa ukiwa mjanja mtaani, na uwe wa kuhifadhi pato lako na usiwe wa kulifuja, ni kwa muda tu kisha ujipate wewe una chako.

“Nimechuuza njugu karanga kwa miaka mitano sasa. Nimeimarika kiasi kwamba nimepata zabuni ya kuuzia idara za serikali bidhaa hizi. Nilianza tu pale mtaani – nikufichulie kuwa ni mtaa wa Zimmerman ukielekea katika jela kuu la Kamiti, kaunti ya Nairobi. Hata ukitaka kuja kujionea karakana yangu ya kupakia bidhaa hizi, kuja na sitakulipisha. Lakini uje ukiwa ushaanza kuchuuza mtaani ndipo uone vile mtu hujiimarisha,” akuahidi.