• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Ongwae akaidi CoG na kuhudhuria kikao bungeni

Ongwae akaidi CoG na kuhudhuria kikao bungeni

Na PETER MBURU

GAVANA wa Kisii James Ongwae Jumatano alikaidi wito wa Baraza la Magavana (CoG) kwa wakuu wa kaunti kuwa wasihudhurie vikao vya Kamati ya Bunge la Seneti Kuhusu Uhasibu, wakati alikihudhuria licha ya kuwa naibu mwenyekiti wa baraza hilo.

Mwenyekiti wa baraza hilo Wycliffe Oparanya wiki mbili zilizopita aliwataka magavana kutohudhuria vikao na kamati hiyo, kufuatia kisa cha Gavana wa Kiambu ambapo alifika mbele ya kamati hiyo huku bajeti yake ikionyesha kuwa serikali ya kaunti ilitoa pesa kufadhili shughuli za serikali kuu.

Ingetarajiwa kuwa Bw Ongwae kwa kuwa ni naibu mwenyekiti wa CoG hangejifikisha mbele ya kamati hiyo, lakini ilikuwa kinyume alipofika mbele yake kujibu maswali kuhusu ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za umma Edward Ouko, kuhusu jinsi Kaunti ya Kisii ilitumia pesa mwaka wa 2017/18.

“Tunashukuru kuwa uliona umuhimu wa kuhudhuria kikao hiki, wala hukufuata wosia wa baadhi ya wenzako ambao walikuwa wakipendekeza magavana wasihudhurie na hilo lina matokeo yake,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo, seneta wa Homa Bay Moses Kajwang.

Gavana huyo aliulizwa na kujibu maswali mbali mbali aliyoulizwa na maseneta kuhusu ripoti hiyo, ambayo Mkaguzi Mkuu alieleza kuwa matumizi ya pesa za umma Kisii yalikuwa kwa njia sawa.

Hata hivyo, licha ya maoni mazuri kutoka kwa Mkaguzi Mkuu kwenye ripoti hiyo, ripoti aidha ilikosoa Kaunti ya kisii kwa kuajiri zaidi ya asilimia 98 ya wafanyakazi wakiwa wa kabila moja, kutumia asilimia 47 ya mapato ya kaunti kulipa wafanyakazi mishahara badala ya asilimia 35 inayopendekezwa kisheria na tofauti kubwa kati ya pesa ilizohifadhi katika benki na zile ilizokusanya kama ushuru.

Vilevile, maseneta walimweka gavana huyo katika kibarua kigumu kueleza jinsi hazina kadhaa zilizoanzishwa na kaunti zilikuwa zikifanya kazi, na ni kwanini Mkaguzi Mkuu hakuzikagua alipokuwa akifanya ukaguzi.

Bw Ongwae, hata hivyo, alijibu na kuridhisha kamati katika mengi ya maswali aliyoangushiwa.

“Baadhi ya tenda amabazo Mkaguzi Mkuu ameibua maswali kuzihusu zilikuwa spesheli na za huduma ambazo hatungetafuta popote tu ila kwa watu mahususi ambao wana ujuzi,” gavana huyo akasema, katika swali aliloulizwa kuhusu kandarasi kadha ambazo kaunti ilitumia mamilioni ya pesa kununua huduma.

You can share this post!

Baadhi ya wadau vita dhidi ya dawa za kulevya walaumu...

Unyakuzi wa ardhi watishia kuangamiza makavazi na turathi

adminleo