• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Kocha mpya wa Malkia Strikers ashinikizwa kutetea ubingwa

Kocha mpya wa Malkia Strikers ashinikizwa kutetea ubingwa

Na JOHN ASHIHUNDU
 
Kocha mpya wa timu ya taifa ya wanawake ya voliboli, Malkia Strikers , Shaileen Ramdoo amewekewa sharti la kuhakikisha timu hiyo imehifadhi ubingwa wa bara Afrika.
 
Ramdoo aliwasili Nairobi mwishoni mwa wiki baada ya Shirikisho la Voliboli Nchini (KVF) kuwasilishwa jina lake kwa Shirikisho la Kimataifa la Voliboli (FIVB) kama mmoja wa maafisa wa kitengo cha kiufundi kwa lengo la kuimarisha mchezo huo nchini.
 
Mkufunzi huyo aliye na vyeti vya FIVB Level 2 na Level 3, tayari ameendesha mafunzo mara mbili kwa timu hiyo ya Malkia Strikers katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani ambapo anatarajiwa kusaidiana na Japheth Munala na David Lung’aho – wakati wa michuano ya Kanda ya Tano ya mchujo wa kufuzu kwa Michezo ya Afrika.
 
Wenyeji Uganda, Kenya, Misri, Tanzania, Rwanda na Ethiopia zimethibitisha kushiriki katika mechi hizo za mchujo zitakazochukuwa wiki moja katika uwanja wa kimataifa wa Lugogo mjini Kampala, mwishoni mwa wiki.
 
“Tuna uhakika wa kutwaa nafasi moja ya kushiriki Michezo ya Afrika mjini Rabat (Morocco) mwezi Augosti,” aliyeleza naibu mwenyekiti Charles Nyaberi.
 
“Ramdoo ni kocha aliye na ujuzi wa kutosha ambaye anaendelea kujifunza mengi kuhusu timu yetu. Tuna uwezo mkubwa wa kuibuka mabingwa huko Kampala lakini kwa sasa lazima turekebishgew makosa kikosini ikizingatiwa kwamba Misri ni miongoni mwa timu kali,” aliongeza mkurugenzi wa wakufunzi, David Lung’aho.
 
Licha ya kutumia wachezaji wengi wa akiba, Kenya iliibuka bingwa wakati wa michezo iliyopita jijini Brazzavill, miaka mine iliyopita.
 
Huenda Ramdoo pia akawa usukani wakati Kenya itakaposhiriki katika Michezo ya Olimpiki mjini Tokyo, Japan mwaka ujao, iwapo watafuzu.
 
Wachezaji ni: Edith Wisa, Emmaculate Chemtai, Joy Luseneka, Pamela Jepkirui, Elizabeth Wanyama, Mercy Moim, Jane Wacu, Triza Atuka, Glady Ekuru, Agrripina Kundu, Sharon Chepchumba, Janet Wanja, Noel Murambi, Leonida Kasaya, Violet Makuto, Lorine Chebet, Jemima Siangu, Linzy Jeruto na Caroline Sirengo.
 

You can share this post!

Migne aeleza sababu za kuwatema mastaa Were na Cheche

Man United itahangaisha wapinzani msimu ujao – Lingard

adminleo