Githu Muigai ainua mikono, Kihara na Ogeto ndani
Na LUCY KILALO
Kwa Muhtasari:
- Yasemekana amejiuzulu kutokana na ukinzani kati ya anachoamini na aliyotakiwa kufanya kisiasa
- Huenda Prof Githu alishauriwa ajiuzulu ili ajiandae kuchukua nafasi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP)
- Akiwa ofisini kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria
JOTO kali katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu limeonekana kuwa sababu kuu ya Profesa Githu Muigai kuamua kujiondoa kwenye wadhifa huo Jumanne.
Wachanganuzi wanaona kuwa Prof Muigai, ambaye amekuwa mshauri mkuu wa serikali katika masuala ya kisheria chini ya Rais Uhuru Kenyatta, amefunganya virago vyake kutokana na ukinzani kati ya anachoamini kama mtaalamu anayeheshimika sana katika taaluma ya sheria na aliyotakiwa kufanya kisiasa.
Mara kadha amekuwa akitoa ushauri, ambao ulipingwa na Wakili Mkuu wa Serikali Bw Njee Muturi, aliyeteuliwa jana kuwa Naibu Mkuu wa Utumishi katika Ikulu chini ya Nzioka Waita.
“Nimepokea kwa masikitiko kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai. Ninamshukuru kwa huduma yake katika kipindi cha miaka sita na nusu iliyopita. Nimemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa Paul Kihara Kariuki, kuchukua nafasi yake,” Rais alitangaza kwenye Twitter.
Nafasi ya DPP
Wachanganuzi wengine wanasema huenda Prof Githu alishauriwa ajiuzulu ili ajiandae kuchukua nafasi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), iliyoachwa wazi na Bw Keriako Tobiko ambaye aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mazingira.
Wanaomfahamu Prof Githu wanasema kama msomi wa masuala ya sheria amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza wanafunzi wake wafuate sheria kikamilifu.
Katika siku za majuzi akiwa ofisini kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria, ikiwemo kukamatwa kwa viongozi wa upinzani na kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani katika muda unaotakiwa.
Vile vile, serikali imeonekana kudharau maagizo ya mahakama, la punde zaidi likiwa ni kuhusu mwanasiasa wa upinzani, Dkt Miguna Miguna.
Mabadiliko mengine
Kwenye mabadiliko mengine aliyotangaza Rais Kenyatta Jumanne, Bw Abdikadir Mohammed, ambaye amekuwa mshauri wake wa masuala ya sheria na kikatiba ametumwa kuwa balozi nchini Korea Kusini.
Wakili aliyemtetea Rais kwenye kesi ya uchaguzi, Kennedy Ogeto naye aliteuliwa Wakili Mkuu wa Serikali kuchukua nafasi ya Bw Muturi.
Rais pia aliwateua aliyekuwa Makamu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Prof Olive Mugenda, aliyekuwa Karani wa Bunge Patrick Gichohi na aliyekuwa waziri wa Kilimo Felix Koskei kuhudumu kama makamishna wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).
Watatu hao sasa watapigwa msasa na Bunge kabla ya kuchuka vyeo hivyo. Umma umepewa siku saba kutuma maoni au pingamizi kuhusiana na watatu hao.
Mnamo Jumatatu jioni, rais aliwateua Bw Charles Hinga Mwaura kuwa katibu wa Nyumba, Bw Kevit Desai (mafunzo ya kiufundi) na Bw Joseph Irungu (Maji na Usafi).