• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
HUDUMA NAMBA: Vijana Baringo wataka walipwe kabla ya kujiandikisha

HUDUMA NAMBA: Vijana Baringo wataka walipwe kabla ya kujiandikisha

NA RICHARD MAOSI
ZOEZI la kujiandikisha kwa Huduma Namba katika Kaunti ya Baringo linaonekana kufeli kutokana na idadi ndogo ya raia waliojitokeza kujisajili kufikia sasa.
 
Kinyume na kaunti nyingine nchini ambapo vijana wamejiandikisha kwa wingi, hali ni tofauti maeneo ya Baringo kwani wazee tu ndio wameitikia amri hiyo ya serikali.
 
Waliosusia zoezi hili ni vijana kati ya miaka 18-28, kwa sababu ya ukosefu wa vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa au pasipoti. Cha kushangaza ni kuwa vijana wengi wamekuwa wakiwaitisha hela mwanzo maafisa wa usajili wakiamini kuwa taarifa kuwahusu ni data ya siri ambayo haifai kujulikana na serikali.
 
Ingawa hiki ni kipindi cha lala salama, shughuli za ufugaji na ukulima, zinaendelea vijijini kama kawaida huku maeneo ya kufanyia biashara yakishuhudia ukame wa watu.
Eneo la Mogotio, Kaunti ya Baringo ambapo idadi ndogo ya watu wamejiandikisha kufikia sasa kutokana na ukosefu wa stakabadhi muhimu. Picha/ Richard Maosi
Taifa Leo Dijitali ilikita kambi katika eneo la Mogotio, kufuatilia zoezi zima ambapo tulikumbana na maafisa wa Huduma Namba wakipiga soga kwenye vituo kwa kukosa watu wa kusajili.  
 
Mmoja wao ni George Komen afisa wa kuandikisha watu ambaye anasema walichukua hatua dharura kuokoa hali, walipochoka kukaa kwenye vituo bila kazi. 
 
Anaeleza kuwa yeye na maafisa wenzake walianza kutembelea nyumba za watu ili kuwabembeleza wajiandikishe wiki ya kwanza wananchi walipodinda kuonekana vituoni.
 
Aidha walipata usumbufu kutoka kwa kundi la vijana, waliokuwa wakiwauliza maswali mengi yasiyokuwa na maana, na hata wengine wakiitisha pesa kwanza kabla ya kujiandikisha, kinyume na wazee ambao walikubali kuchukua huduma namba bila maswali mengi.
Maafisa wa kuandikisha raia huduma namba wakiwa wamebarizi wakisubiri kuhesabu siku kutokana na uhaba wa watu. Picha/ Richard Maosi
Bw Komen anasema usumbufu kutoka kwa vijana ulikuwa mwingi, nusura ufanye wakate tamaa.
 
“Vijana wengi hapa hawakuendeleza masomo yao zaidi ya shule ya msingi, labda ndio sababu wanaamini serikali haina mipango ya kuwafaidi siku za mbeleni,” alisema.
 
Zaidi ya asilimia 80 ya wakazi hawana stakabadhi za kujisajili, wengi wao wamepiga foleni katika kambi za chifu kutafuta vitambulisho kwanza kabla ya kujiandikisha.
 
Mama Ann Chepkosgei muuzaji matikiti maji anasema haoni haja ya kuchukua Huduma Namba kwa sababu wakazi wa Baringo wamekuwa wakipuuzwa.
 
Anasema Kaunti ya Baringo imekuwa ikitengwa na serikali ya kitaifa, wala hakuna miradi yoyote iliyoanzishwa kuleta maendeleo. 
 
“Watu wengi hapa wameridhia hali ngumu ya maisha, kwa mfano mpaka sasa tunatumia lami aliyounda mkoloni huku tukitaabika kupata chakula,” alisema.
 
Lakini anaona zoezi hili liratibiwe upya kwa kuonyesha maslahi kwa baadhi ya watoto waliozaliwa lakini wazazi wao wakaaga dunia.
Vifaa hivi vya kusajili data kidijitali vimesalia bila kazi katika maeneo mengi ya Baringo. Picha/ Richard Maosi
 
“Hawana mbinu ya kupata vyeti vya kuzaliwa, kwani waliachwa chini ya ulezi wa mababu zao ambao hawajui pa kutafuta stakabadhi hizi,” aliongezea.
 
Ingawa eneo la Marigat lina idadi ndogo ya wakazi, huenda wakazi wameona heri kufanya shughuli nyingine kama kulinda mifugo.
Chifu wa Midwell, kaunti ndogo ya Mogotio John Bundotich, anajuta laiti vijana wangefahamu umuhimu wa kujiandikisha kwa Huduma Namba.
 
“Wengi wao tangu waachane na shule walijiingiza kwenye biashara za kuuza asali na pesa walizopata wakazitumia kunywa pombe ,” alisema.
 
Lakini kinachomtia wasiwasi ni ikiwa serikali itawapa wakazi wa Mogotio fursa ya kutafuta vitambulisho au vyeti vya kuzaliwa muda wa kujiandikisha ukiisha.
Wengi waliojisajili ni wazee ilhali vijana wametorokea vijijini ili kukwepa shughuli za kujiandikisha.

You can share this post!

Korti yakataa rufaa ya mzee aliyefungwa maisha kwa...

SRC yataka wabunge warejeshe marupurupu

adminleo