Matiang'i aahidi kumaliza genge la mauaji eneo la Matungu
Na MWANGI MUIRURI
WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amefichua Alhamisi kuwa mshirikishi wa mauaji ya kikatili katika eneo la Matungu Kaunti ya
Kakamega ni jambazi sugu ambaye alitoroka jela baada ya kwamba alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani.
“Alitoroka kutoka gereza la Kamiti na akiwa katika maficho yake katika Kaunti ya Nairobi, amekuwa akishirikisha mauaji haya. Lakini mtego wetu kama serikali umemnasa na kwa sasa anajumuika na wengine kadhaa ambao tumetia mbaroni na ambao wanatusaidia na uchunguzi,” amesema Matiang’i.
Dkt Matiang’i aidha amesema ana habari kuhusu washukiwa wengine ambao kwa muda wa wiki tatu sasa wamekuwa wakihangaisha wakazi
wa eneo hilo na ambapo tayari watu 14 wameripotiwa kuuawa na genge la uvamizi.
Alipozuru eneo hilo akiandamana na wakuu kadhaa wa vitengo vya usalama katika kaunti hiyo na eneo pana la Magharibi sambamba na waratibu wa masuala ya kiusalama katika wizara na Ikulu, Dkt Matiang’i amemtaka yeyote anayejua kwamba anahusika na mauaji hayo ajisalimishe mikoni mwa serikali.
“Ukiwa wewe unajielewa sawasawa na unajua unashiriki mauaji haya, nakuomba tu ujisalimishe kwa maafisa wa usalama,” ameonya Matiang’i.
Ametoa onyo hilo akiwataka washukiwa hao waelewe kuwa siku zao za mchezo wa paka na panya katika ujambazi wa eneo hilo zimefika kikomo.
“Mimi natoa hakikisho hili. Hakuna tena kuhangaisha wananchi hapa Matungu au kwingineko. Sahau na usahau kabisa. Mimi ndiye ninakuambia hivyo hapa hadharani,” akasema.
Alisema kuwa mikakati ile imewekwa inahusisha uhamisho wa maafisa wa usalama eneo hilo, kuwatuma wengine ambao wamepewa amri za moja kwa moja kukabiliana na hali hiyo na hatimaye kuwekwa vikosi spesheli vya GSU ili kumenyana sawasawa na wavamizi hao.
“Ujumbe wangu kwa wavamizi hawa ni kuwa wametuitia kazi… Mmetuitia kazi, tuonane basi,” akasema katika hali ya kukubali mwito wa wananchi
ambao wamekuwa wakiteta kuwa eneo hilo limekuwa kama limetelekezwa na serikali na kutawaliwa na ‘serikali ya ujambazi’.
Mara zote Matiang’i ametoa hakikisho hilo akizuru eneo tata, kama alivyofanya hizi majuzi katika Kaunti ya Nyeri ambapo genge lilikuwa
likiua maafisa wa serikali kiholela, maafisa huwa wanazingatia maelekezo hayo na shida huwa inaisha.
Kujadiliana
Dkt Matiang’i amesema amekuwa akijadiliana na viongozi wa eneo hilo la Matungu na ambapo wote wamekubaliana kuhusu mikakati ya
kurejesha usalama eneo hilo.
Ingawa kumekuwa na tetesi kuwa kuna uwezekano wa ushirika wa wanasiasa watatu katika ghasia hizo za mauti, waziri Matiang’i hakughusia madai hayo, akionya tu kuwa “hata iwe ni nani katika ngoma hii ya ujambazi, tutamshughulikia kama jambazi wa kawaida.”
Wenyeji wamekuwa na shida kubwa na ambapo wamekuwa wakilia serikali haionekani kuwajali na katika msingi huo, vijana wa eneo hilo wamekuwa
wakilipiza kisasi ambapo tayari nao wameua washukiwa yapata watano kwa kuwapiga kwa mawe na kisha kuwateketeza.
Waziri Matiang’i amesema kuwa hali sawa na hiyo ilikuwa imezuka mwaka 2018 katika eneo jirani la Mlima Elgon na ambapo genge lilichipuka na
kuendeleza mauaji ya kikatili.
“Nilitua huko na nikatoa onyo, nikaahidi kurejesha amani na hadi sasa huko kumetulia tuli. Tutatumia mbinu sawa na iliyotumika hapo na nawahakikishia hapa Matungu kutanyamaa. Nawaambia mimi kama waziri hapa hadharani kuwa mtalala kwa amani na mtaamka kwa amani. Hilo msiwe na shaka nalo kwa kuwa ni serikali sasa imesema,” akasema.