Habari Mseto

HUDUMA NAMBA: Wakenya waililia serikali iwaongezee muda

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Je, umejisajili kwa Huduma Namba? Iwapo hujafanya hivyo, siku za kukunja jamvi shughuli hii zinabisha hodi.

Siku ya mwisho kujisajili ni mnamo Jumamosi, Mei 18, mwaka huu, serikali ikishikilia kuwa haitaongeza muda.

Wanaoishi ughaibuni, pia wanajisajili ambapo zoezi hilo lilianza May 6 na linatarajiwa kutamatika Juni 19.

Kulingana na Waziri wa Usalama Ndani na Mikakati ya Serikali ya Kitaifa Dkt Fred Matiang’i, kufikia Jumatatu wiki hii watu milioni 31 ndio walikuwa wamejisajili.

“Hatutaongeza muda zaidi wa kujisalili. Ukitamatika, machifu watasalia na fomu na utakuwa na wakati mgumu kuwatafuta kwani nao pia wana majukumu mengine waliyotwikwa na serikali,” Waziri Matiang’i alisema mnamo Jumatatu.

Alisisitiza kwamba ili kupokea huduma za serikali kwa urahisi, mwananchi atahitajika kutumia Huduma Namba. “Huduma za serikali zitarahisishwa kupitia Huduma Namba. Wewe ndiye utaamua iwapo unataka kutumia njia ndefu kuzipokea,” alieleza.

Kwa mujibu wa marekebisho ya kipengele cha katiba cha usajili wa watu kifungu cha 9A yaliyofanyika 2018, Wakenya wote na raia wa kigeni walioko nchini, wanapaswa kusajiliwa katika mpango wa kitaifa kupitia mfumo wa NIIMS (National Integrated Identity Management System).

Serikali inahoji kuwa mpango huu ni muhimu katika upangaji wa mikakati yake, utoaji na usambazaji wa huduma, utoaji wa raslimali za umma pamoja na maendeleo.

Huku muda ukiyoyoma, vituo vya usajili wiki hii vimeonekana kupokea idadi kubwa ya watu kutokana na milolongo mirefu inayoshuhudiwa.

Kwa kawaida, hapa nchini watu hukimbia wakati wa mwisho ili kutekeleza matakwa ya aina hiyo. Kwa mfano, wakati wa kujisajili kuwa mpiga kura, imekuwa mazoea Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka (IEBC) kupokea idadi kubwa ya watu siku za mwishomwisho.

Katika uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali vituo kadhaa tulivyozuru kaunti ya Nairobi na Kiambu, laini ndefu za watu waliojitokeza kujisali wiki hii zimeshuhudiwa.

“Wengi wetu hutoka kazini kama tumechelewa na tunaomba serikali ituongezee muda kwa sababu ya laini ndefu zilizoko,” akasema mkazi mmoja wa Zimmerman, Nairobi na aliyeomba kubana jina lake.

Simon Kagombe, mfanyabiashara mtaani Githurai 45, Kiambu, naye amesema wiki hii jitahada zake kujisajili zimegonga mwamba kwa ajili ya idadi kubwa ya watu. “Hata hivyo, lazima nijisajili kabla zoezi lenyewe kukamilika,” akasema.

Baadhi ya vituo nchini vimeripotiwa kuwa na upungufu wa fomu za usajili, na kwingine mashine za mtambo wa BVR zikiwa chache na zingine kukwama.

Serikali imehakikishia wananchi kuwa data zinazonakiliwa zitakuwa salama, kutokana na hofu ya baadhi ya Wakenya.

Ili kusajiliwa, unapaswa kujiwasilisha katika kituo cha kujisajili. Wenye umri wa miaka 18 na zaidi, wanahitajika kuwa na kitambulisho cha kitaifa, huku walio chini ya umri huo wakipaswa kutoa cheti cha kuzaliwa.

Pia, ikiwa stakabadhi kama leseni ya kuendesha gari, kadi ya NSSF, bima ya afya NHIF na nambari ya halmashauri ya utozaji ushuru KRA, unahimizwa kuziwasilisha.