Marwa kusimamia Kombe la Dunia Urusi
Na GEOFFREY ANENE
REFA bora wa mwaka wa kunyanyua kibendera nchini Kenya mwaka 2017, Aden Range Marwa amejumuishwa katika orodha itakayokuwa katika Kombe la Dunia nchini Urusi mnamo Juni 14 hadi Julai 15, 2018.
Marwa, ambaye ni mwalimu wa somo la hisabati na kemia katika shule moja ya upili kutoka Kaunti ya Migori, ni Mkenya pekee katika orodha hiyo.
Marefa waliochaguliwa kutoka Afrika na Shirikisho la Soka duniani (FIFA) ni Grisha Ghead (Misri), Abid Charef Mehdi (Algeria), Sikazwe Janny (Zambia), Tessema Weyesa Bamlak (Ethiopia), Diedhiou Malang (Senegal) na refa bora Barani Afrika mwaka 2014, 2015 na 2016 Gassama Bakary Papa (Gambia).
Marefa wasaidizi (wanyanyuaji vibendera) ni Etchiali Abdelhak (Algeria), Hmila Anouar (Tunisia), Camara Djibril (Senegal), Samba El Hadji Malick (Senegal), Birumushahu Jean Claude (Burundi), Aden Range Marwa (Kenya), Achik Redouane (Morocco), Ahmed Waleed (Sudan), Dos Santos Jerson Emiliano (Angola), Siwela Zakhele Thusi (Afrika Kusini), Safari Olivier (Ivory Coast) na Ssonko Mark (Uganda).
Timu za taifa za Misri, Tunisia, Morocco, Senegal na Nigeria zilifuzu kuwakilisha Bara Afrika nchini Urusi. Mataifa 32 yatashiriki Kombe la Dunia ambapo mechi 64 zitasakatwa katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.