Michezo

Malkia Strikers watakaosafiri Kampala watajwa

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

GEOFFREY ANENE NA JOHN ASHIHUNDU

MABINGWA wa voliboli ya wanawake barani Afrika ya mashindano ya All-Africa, Kenya wametaja kikosi cha wachezaji 12 watakaoitafutia tiketi ya kutetea taji katika mchujo wa ukanda wa tano jijini Kampala, Uganda kutoka Mei 18-25, 2019.

Kocha Japheth Munala ameweka imani yake kwa wachezaji wazoefu wakiwemo Janet Wanja, Mercy Moim, Noel Murambi, Triza Atuka na Edith Wisa walioshiriki mchujo wa kuingia makala ya mwaka 2015.

Timu ya Kenya, ambayo imekuwa ikifanyia mazoezi yake katika ukumbi wa kimataifa wa Kasarani, inatarajiwa kuelekea nchini Uganda hapo Ijumaa kwa mashindano haya ambayo mshindi atafuzu kushiriki makala hayo ya 12 mjini Rabat nchini Morocco. Nchini Uganda, Kenya itakutana na wenyeji Uganda, mahasimu wa tangu jadi Misri pamoja na Rwanda, Tanzania na Ethiopia.

Ni timu moja pekee itakayopata tiketi ya kwenda Morocco kuwania ubingwa wa Afrika wakati wa Michezo ya Afrika itafayofanyika mjini Rabat mwezi Septemba.

“Hatogopi timu yoyote kwa vile tumejiandaa vyema kwa mbinu mbali mbali za kutowezesha kuhifadhi ubingwa,” alisema nahodha Moim anayechezea klabu ya Supreme nchini Thailand.

Kadhalika, Japheth Munala atakayesaidiana na Ramdoo anaitarajia timu hiyo kuandikisha matokeo mema katika mechi zao baada ya maandalizi mema.

“Ujio wa Ramdoo umeiongezea timu hii nguvu nyingi na sasa tuko tayari kabisa kukabiliana timu yeyote ikiwemo Misri ambao ndio wapinzani wetu wakuu,” aliongeza.

Miongoni mwa wachezaji walio kikosini ni pamoja na Edith Wisa na Triza Atuka ambao huchezea klabu za Magereza na Kenya Pipeline pamoja na mshambuliaji matata, Immaculate Chemtai.

Kenya walitwaa ubingwa wa Michezo ya Afrika msimu uliopita baada ya kuwabwaga Algeria, wenyeji Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Cameroon mjini Brazzaville miaka mine iliyopita.

Wachezaji walio kikosini ni: Jane Wacu, Janet Wanja, Mercy Moim, Leonida Kasaya, Sharon Chepchumba, Noel Murambi, Lorine Chebet, Edith Wisa, Trizah Atuka, Violet Makuto, Emmaculate Chemtai na Agrippina Kundu.

Kikosi cha Malkia Strikers (2019):

Maseta – Jane Wacu, Janet Wanja; Washambuliaji wa pembeni kushoto – Mercy Moim (nahodha), Leonida Kasaya, Sharon Chepchumba, Noel Murambi; Wazuiaji wa kati – Lorine Chebet, Edith Wisa,Triza Atuka; Washambuliaji wa pembeni kulia – Violet Makuto, Emaculate Chemtai; Libero – Agripina Kundu. Benchi la kiufundi: Kocha – Shailene Shamdoo (Italia), Kocha – Japheth Munala, Kocha – Josp Barasa.