Habari

Al-Shabaab wageuza madaktari wa Cuba watumwa wao

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

AMINA WAKO na MASHIRIKA

MADAKTARI wa Cuba waliotekwa nyara katika Kaunti ya Mandera na kundi la kigaidi la Al-Shabaab, wamefanywa watumwa katika ngome inayosimamiwa na magaidi hao, duru za kuaminika zimesema.

Wazee wa jamii ya Kisomali ambao walienda katika kijiji cha Jubbaland, Somalia ambako Dkt Assel Herera Corea na Dkt Landy Rodriguez wanaaminika kushikwa mateka, walifichua kuwa al-Shabaab inataka kulipwa Sh150 milioni ndipo madaktari hao waachiliwe huru.

Alhamisi, walithibitisha kwamba madaktari hao wangali hai ingawa wamelazimishwa na Al-Shabaab kutoa matibabu kwa jamii zinazoishi katika eneo linalosimamiwa na magaidi nchini Somalia.

Wazee hao kutoka Mandera nchini Kenya na Bulahawo nchini Somalia, walikuwa wametumwa na serikali ya Kenya katika kijiji hicho kilicho kati ya maeneo ya Buale na El-Adde, kufanya mazungumzo na kundi hilo la kigaidi ili kupata maelewano ya kuwaachilia madaktari hao wawili.

Katika jamii ya Kisomali, wazee wa kijamii huchukuliwa kwa umuhimu mkubwa na wenye uwezo wa kutatua masuala mazito ambayo wakati mwingine pia huwa hatari.

Madaktari hao walitekwa nyara mnamo Aprili 12 karibu na mpaka wa Kenya na Somalia. Mmoja wa maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakiwalinda alipigwa risasi na akafariki kisha wavamizi wakatorokea Somalia.

Afisa wa ngazi za juu serikalini katika Kaunti ya Mandera alithibitisha watekaji nyara wanataka kulipwa fidia, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu hatua zilizopigwa kufikia sasa.

“Kiwango cha fedha wanachotaka ni Sh150 milioni. Huo ndio msimamo wao,” akasema afisa huyo aliyeomba asitajwe jina.

Afisa wa polisi mwenye cheo cha juu pia aliambia shirika la habari la AFP kwamba watekaji nyara wameitisha fedha, ingawa msemaji wa polisi, Bw Charles Owino alisema hajapokea habari hizo.

Madaktari hao ni miongoni mwa wengine 100 kutoka Cuba ambao waliletwa Kenya mwaka uliopita kuboresha utoaji wa huduma maalumu za matibabu katika kila kaunti.

Kufuatia kisa hicho cha utekaji nyara, serikali iliagiza madaktari wa Cuba waliokuwa wamepelekwa kaunti za Wajir, Lamu, Garissa na Tana River, ambazo zimepakana na Somalia, warudishwe Nairobi kwa usalama wao. Madaktari hao walipelekwa kuhudumu katika kaunti zingine.