Uhuru aona moto
Na PETER MBURU
RAIS Uhuru Kenyatta ameendelea kukashifiwa na wananchi kwenye mitandao ya kijamii, wakieleza hisia zao kali kwa kile wanachokiona kama serikali kutojali maslahi yao.
Jumbe hizi zimefurika hasa kwenye Facebook na Twitter na nyingi zimejaa ukali, machungu na hisia za kupoteza matumaini.
Rais alipoondoka nchini Jumatano kuelekea Rwanda kuhudhuria kongamano, watumiaji wengi wa mitandao walishangaa jinsi Kenya itakavyofaidika kutokana na ziara hiyo.
Jumbe hizo zilionyesha hasira za Wakenya, sio kwa kwenda Rwanda, mbali kutokana na hatua kadhaa ambazo Serikali imechukua katika kipindi chake cha pili cha uongozi, ambazo zimeonekana kunyanyasa Mkenya wa kawaida.
Baadhi ya hatua ambazo zimeonekana kuwakera wengi ni ufisadi mkubwa serikalini, VAT ya petroli mwaka jana, ukopaji wa mabilioni ya pesa kutoka China, mpango wa kuwatoza wafanyikazi ushuru wa kufadhili ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na usajili wa ‘Huduma Namba’.
Kukashifiwa huku kwa Rais Kenyatta kumeongezeka tangu alipoafikiana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, hatua ambayo ilimfunga kinywa kutetea maslahi ya raia wa kawaida.
Tangu hapo, utengano kati ya Rais Kenyatta na wananchi umezidi kwani sasa wanalazimika kujitetea wenyewe serikali inapochukua hatua wanazohisi si za haki.
Mitandao ya kijamii imekuwa sehemu kubwa ya Wakenya kupaza sauti kupinga mambo yanayowaudhi katika serikali na hata mashirika mengine ama masuala ya kijamii, lakini hasa imekuwa kipaza sauti muhimu kuhusu masuala ya uongozi nchini.
Mavuguvugu ya mitandaoni yamekuwa na mchango mkubwa kwa kulalamikia masuala ambayo hayaendi sawa, na mara kadhaa yameifanya serikali ama mashirika mengine kujitokeza kurekebisha mambo ama kufafanua kuhusu masuala ambayo yanalalamikiwa.
“Kulingana na madeni ambayo amekopa, sidhani ana uwezo wa kubadilisha Afrika, labda awe anapiga Kenya mnada,” Ngechu Jackson akasema katika mtandao wa Facebook.
“Tafadhali Kagame kaa naye kwa miaka mitatu ijayo, ametuchosha,” haya yalikuwa maneno ya Kamau Wanjiru kwenye Twitter kuhusu ziara ya Rais Kenyatta nchini Rwanda.
“Tafadhali muulize Kagame jinsi ameweza kuendesha Rwanda kwa utulivu bila rasilimali za umma kuporwa ama ufisadi. Huenda kutokana na ushauri wake ukafanikiwa kutimiza malengo yako,” akasema mtumizi mwingine.
Hali hii ya Wakenya kumshambulia Rais mara kwa mara kila anapozungumza imekuwa na athari zake kwani takriban miezi miwili iliyopita, akaunti zake za mitandao ya kijamii zilifungwa na hadi sasa hazijarejeshwa.
Kabla ya hatua hiyo, Wakenya walikuwa wakielekeza matusi ya aina zote.
Ilikuwa imefikia kiwango kuwa hata alipohutubu na kusema kuwa anazungumza “kwa niaba ya Wakenya”, watumizi wa mitandao walimkosoa na kusema hawataki awawakilishe.