Yafichuka familia ya Moi iliogopa Huduma Namba
Na BENSON MATHEKA
FAMILIA ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi ilihofia kujisajili kwa Huduma Namba ikishuku mambo yao ya siri hayangekuwa salama, imefichuka.
Seneta wa Baringo Gideon Moi, ambaye ni mwanawe Mzee Moi, amekiri kwamba walikuwa miongoni mwa Wakenya ambao walijiuliza maswali mengi kuhusu nia ya serikali kutaka watu wajisajili kupata Huduma Namba.
Akihutubu Ijumaa wakati wa maadhimisho ya siku ya mawasiliano na utandawazi jijini Nairobi, Seneta Moi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano alisema yeye na familia yake hawakuwa wakiamini habari zao zitakuwa salama.
Mzee Moi alijisajili jana nyumbani kwake Kabarnet Gardens, Nairobi akiwa pamoja na seneta huyo na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Bw Joe Mucheru.
“Ninataka kusema kwamba nilikuwa mmoja wa wale walioogopa kuchukua huduma namba kwa sababu sikuwa na hakika ikiwa habari kunihusu zingekuwa salama. Nilikuwa naogopa lakini baada ya wizara kunihakikisha kuna sheria ya kulinda habari za Wakenya, tuliamua kujisajili,” akasema Bw Moi.
Alisema baada ya kupata maelezo kutoka kwa wizara ya teknolojia na mawasiliano aliamua kujisajili.
Bw Moi alishukuru wizara ya tekinolojia kwa kushirikiana na seneti wakati wa kuandaa sheria ya kulinda habari mtandaoni ya 2018.
“Ni muhimu Wakenya kuhakikishiwa usalama wa habari zao za kibinafsi na sheria ya kulinda habari ya 2018 inastahili kuzingatiwa,” alisema.
Ijumaa, watu walijitokeza kwa maelfu katika vituo kujisajili kupata huduma namba siku mbili kabla ya muda wa siku 45 uliotolewa na serikali kukamilika.
Taarifa ya kutoka Ikulu iliyofuata baadaye imesema Rais Uhuru Kenyatta ameagiza kuongezwa wiki moja zaidi Wakenya wasajiliwe.
Shughuli hiyo itakamilika Jumamosi, Mei 25, 2019.
Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alisema watu 35 milioni walikuwa wamesajiliwa kufikia Ijumaa.
Awali Chama Cha Wanasheria nchini (LSK) kilisema hakuna Mkenya anayepaswa kuzuiwa kujisajili au kulazimishwa kujisajili.
Kwenye taarifa, mwenyekiti wa chama hicho Allen Gichuhi alisema kilipata agizo la Mahakama kuzuia serikali kulazimisha watu kusajiliwa na kunyimwa huduma kwa kukosa kusajiliwa.