Rais Kenyatta aagiza shughuli ya usajili wa Huduma Namba iendelee kwa wiki moja zaidi
Na CHARLES WASONGA na PSCU
WAKENYA ambao walikuwa hawajisajili kwa Huduma Namba kwa sababu moja ama nyingine, wamepata afueni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuongeza muda wa usajili kwa wiki moja zaidi.
Hii ina maana kuwa shughuli hiyo ambayo ilipaswa kufikia kikomo Jumamosi, Mei 18, 2019, sasa itaendelea mpaka Jumamosi Mei 25, 2019.
Mnamo Ijumaa foleni ndefu zilishuhudiwa kote nchini huku watu wakipania kujisajili kabla ya siku ya mwisho kufika.
Baadhi ya watu walikosa kwenda kazini na watoto wakikosa kwenda shuleni ili wapate muda wa kwenda katika vituo vya usajili.
Katika taarifa kutoka Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta alisema ameamuru Kamati ya Mawaziri Inayoshirikisha Mipango kuongeza muda wa usajili wa Huduma Namba kwa wiki moja zaidi.
Wakati huo huo Rais alisema kuwa usajili wa Wakenya wanaoishi ughaibuni ulioanza Mei 6 katika balozi za Kenya utaendelea hadi Juni 20 mwaka huu.
“Ningependa kuwashukuru vijana 42,000 wanaofanya kazi kama Wasaidizi wa Usajili na Maafisa 8000 wa Usajili na maafisa 400 wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano waliohudumu katika kaunti zote ndogo nchini,” akasema Rais Kenyatta.
“Hata hivyo, nimeangalia na kuona foleni ndefu wakati wa siku hizi za mwisho za zoezi hili katika sehemu mbali mbali za nchi. Hii inadhihirisha tabia yetu ya kushughulikia mambo saa za mwisho jambo ambalo limeendelea kutuzuia kupiga hatua. Hata hivyo, Wakenya wamejitolea kujisajili kupata Huduma Namba na nimekubali maombi yao ya kuwapa muda zaidi kufanya hivyo,” akaeleza.
“Hivyo basi naiagiza kamati inayojumuisha wizara husika za kitaifa inayohusika na utekelezaji mpango huu kuongeza muda wa usajili kwa wiki moja zaidi. Hii ina maana kuwa shughuli hii itakamilika mnamo siku ya Jumamosi, Mei 25 saa kumi na mbili jioni,” Rais Kenyatta akasisitiza.
Kiongozi wa taifa aliwahimiza wale ambao hawajajisajili kutumia kikamilifu muda huu wa ziada wajisajili badala ya kusubiri hadi siku ya mwisho.