• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
ODM kuadhibu ‘waliopanga’ kumzoma Raila

ODM kuadhibu ‘waliopanga’ kumzoma Raila

Na RUSHDIE OUDIA

CHAMA cha ODM kimeapa kuadhibu vikali wahusika waliosababisha kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga kuzomwa wakati alipozuru eneo la Ombei, Muhoroni mnamo Jumatatu iliyopita ikiwa itathibitishwa ni wanachama wa ODM.

Chama hicho kimesema kimeanzisha upelelezi ili kubainisha aliyepanga tukio hilo na ikipatikana ni kiongozi aliyechaguliwa kwa tikiti ya ODM, ataadhibiwa ipasavyo.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na mawaziri James Macharia (Uchukuzi na Miundomsingi), Peter Munya (Biashara na Viwanda) na John Munyes (Mafuta na Madini) kwenye ziara ya eneo lililopendekezwa kuwa eneo maalumu la kiuchumi wakati kisa hicho kilipotokea.

Vijana waliokuwa na mabango walianza kupiga kelele na kuzoma wakisema hawataki ardhi zao zitumiwe kama eneo maalumu la kiuchumi na serikali.

Bw Odinga alikuwa ametangaza mradi huo wa serikali kuu umenuiwa kugeuza Muhoroni kuwa kitovu cha uwekezaji katika Kaunti ya Kisumu na itakuwa baraka kwa wakazi kwani watapata nafasi za ajira.

Lakini vijana hao walidai hiyo ni njama ya serikali ya kaunti kunyakua ardhi zao bila kushauriana nao kwanza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa ODM katika Kaunti ya Kisumu, Prof Ayiecho Olweny alidai vijana hao wabishi ni watu wanaofahamika vyema Muhoroni lakini si wa jamii ya Sidho inayomiliki ardhi husika.

“Walionekana wakipewa mabango kutoka kwa gari hata kabla hafla kuanza. Hatutaacha suala hili litokomee bila kupata wahusika,” akasema Prof Olweny.

Viongozi wakashifiwa

Alikashifu pia viongozi wa Kaunti ya Kisumu kwa kutohudhuria hafla hiyo ambayo umuhimu wake uliashiriwa na kuwepo kwa Bw Odinga na mawaziri watatu wa serikali kuu.

Viongozi wa kaunti waliokuwepo ni Naibu Gavana Mathews Owili, Seneta Maalumu Rose Nyamunga, na Mbunge wa Nyando Jared Okello. Mbunge wa Rarieda, Bw Otiende Amollo pia alikuwepo.

Prof Olweny alisema itakuwa vyema mradi unaolengwa uanzishwe mara moja kwa manufaa ya jamii.

“Haiwezekani kila siku tunabaki nyuma kwa sababu tunakataa kila mradi wa maendeleo tunaoletewa,” akasema.

Wakati wa hafla hiyo, Gavana Anyang’ Nyong’o alikuwa Denmark naye Mbunge wa eneo hilo, Bw Onyango K’Oyoo alikuwa Botswana kikazi.

Wawili hao walikemea wakazi wanaopinga mradi huo na wakasisitiza kisa kilichoshuhudiwa kilikuwa kimepangwa mapema.

“Inasikitisha kuwa kundi dogo la watu ambao wameamua hawataki maendeleo katika kaunti nzima kwa manufaa yao ya kisiasa waliamua kuaibisha wageni wetu,” alisema Prof Nyong’o, huku akiwakemea kuwa ni watu wasiokuwa na maono.

Bw K’Oyoo alishangaa kwa nini maafisa wakuu wa chama katika kaunti hiyo walikosa kuchukua hatua kuzuia kisa hicho.

“Inasikitisha sana na hili ni tukio ambalo kamwe halikustahili kushuhudiwa hasa kwa kiongozi wa chama chetu. Tunakikemea zaidi,” akasema.

Kwa upande wake, Mweka Hazina wa ODM katika tawi la Kisumu, Bw Festus Achilla alisema polisi wangekamata wahusika kwani tukio hilo lilifanyika mbele yao.

You can share this post!

Usajili: Agizo la Rais lafanya wengi kulegea

Malkia Strikers yatua Uganda baada ya nuhusi ya kusubiri...

adminleo