• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
Kenya tayari kutetea ubingwa wa voliboli ya wanawake Afrika

Kenya tayari kutetea ubingwa wa voliboli ya wanawake Afrika

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya iko tayari kutetea ubingwa wa voliboli ya wanawake ya Afrika ya Ukanda wa Tano itakayoanza jijini Kampala nchini Uganda hapo Mei 19, 2019.

Katika mahojiano na mmoja wa makocha wa timu hiyo maarufu kama Malkia Strikers, Josp Barasa alisema, “Tuko tayari kwa mechi yetu ya ufunguzi dhidi ya Rwanda. Rwanda ni timu nzuri na hatuwezi kuchukulia mechi hiyo kwa mzaha. Mechi za kwanza mara nyingi huwa ngumu, lakini tuko tayari kuwakabili.”

Kocha wa kimataifa Sammy Mulinge, ambaye pia ni Mkenya, alibashiri mechi hii itakuwa na msisimko wa aina yake.

“Hii mechi ya Rwanda na Kenya itakuwa ya kusisimua sana kwani Rwanda itakuwa inataka kupatia mibabe wa Afrika ambao ni Kenya, ushindani mkali. Kenya iko mguu moja mbele kwa sababu ya uzoefu wake wa kucheza michezo mingi hapa Afrika na nje ya Afrika. Hata hivyo, timu ya Rwanda inajivunia misingi ya usaidizi mkubwa kutoka kwa serikali ya nchi yake, basi inataka kuweka bidii yake yote katika mashindano haya. Kukosekana kwa timu ya Misri, kila mmoja atakuwa na nafasi nzuri ya kugombea tiketi hiyo moja ya kuelekea nchini Morocco kwa mashindano ya All-African.”

Kenya ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kuwasili nchini Uganda, licha ya kuwa ilisafari saa 24 baada ya muda ilikuwa imepangiwa.

Ethiopia na Rwanda zilitarajiwa jijini Kampala baadaye Jumamosi. Kuchelewa kwa timu hizi mbili kulisababisha mkutano wa kiufundi unaofanyika siku moja kabla ya mashindano kuanza, uahirishwe hadi Jumapili asubuhi.

Mshindi wa mashindano haya atafuzu kushiriki mashindano ya All-African yatakayoandaliwa jijini Rabat kutoka Agosti 19-31, 2019.

Kikosi cha Kenya

Mercy Moim, Sharon Chepchumba, Noel Murambi, Leonida Kasaya, Violet Makuto, Immaculate Chemutai, Jane Wacu, Janet Wanja, Edith Wisa, Triza Atuka, Lorine Chebet na Agripina Kundu.

You can share this post!

KENYA CUP: KCB yadunga Kabras Sugar mwiba mchungu katika...

UFUGAJI: Masuala muhimu kuzingatia kabla kuanza kufuga kuku

adminleo