• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
UFISADI: Rais asiyeweza kung’ata atisha tena

UFISADI: Rais asiyeweza kung’ata atisha tena

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta kwa mara nyingine ametoa vitisho vikali dhidi ya wanaohujumu vita vya kupambana na ufisadi. Ila swali ni je, mara hii atachukua hatua kali, ama ni vitisho vitupu tu vilivyozoeleka?

Juma moja baada ya viongozi wa Kanisa Katoliki kueleza wasiwasi kwamba juhudi za kuangamiza ufisadi zimefifia, Rais alitumia mkutano wake na mabalozi wa mataifa ya Jumuiya ya Ulaya (EU) kusisitiza kuwa moto wa kuangamiza wizi wa mali ya umma ungali unawaka.

Mkutano huo wa Ijumaa ulihudhuriwa pia na naibu wake, Dkt William Ruto pamoja na mawaziri kadhaa katika Ikulu ya Nairobi.

“Tutaendelea kupiga vita ufisadi bila kujali kinachosemwa wala kufanywa. Inasikitisha kuna wakati ambapo juhudi hizi huingiziwa siasa lakini kama nilivyosema, hivi ni vita ambavyo lazima Kenya ishinde,” akasema.

Rais alisisitiza: “Hii itafanyika. Haitakuwa rahisi, kelele zitakuwapo lakini itafanyika, itafanyika itafanyika. Hakuna kurudi nyuma.”

Kwenye kikao hicho, wajumbe wa EU walitangaza kujitolea kwao kusaidia taifa hili kufanikisha malengo yake ya kuangamiza ufisadi kwa manufaa ya wananchi.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (KCCB) Philip Anyolo, viongozi wa kanisa hilo walikuwa wamelalamikia jinsi vita dhidi ya ufisadi vilivyoingizwa siasa kwa kiasi cha kufanya vififie.

Kesi nyingi zinazohusisha ufujaji wa pesa katika mashirika mbalimbali ya serikali zimefikishwa mahakamani kufikia sasa lakini hakuna hatua kubwa iliyopigwa kuziendeleza mbele.

Vilevile, wananchi wengi walitarajia Rais kutangaza jambo kubwa kuhusu vita dhidi ya ufisadi wakati alipotoa hotuba ya hali ya taifa bungeni mwezi uliopita.

Ilitarajiwa pengine angesimamisha kazi mawaziri wapatao sita waliohusishwa na ufisadi lakini badala yake ikawa ni vitisho vitupu kwa mara nyingine.

Ijumaa, Rais Kenyatta alisisitiza, kwa mara nyingine tena, kwamba hatalegeza msimamo katika kupambana na ufisadi hata kama kuna pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi.

“Tunajua kuna wale ambao wanajitahidi kuhujumu juhudi zinazofanywa kuangamiza ufisadi ili turudie jinsi hali ilivyokuwa zamani. Hatutapumbazwa na sarakasi zao,” Rais Kenyatta akaongeza.

Hayo yalijiri huku Naibu Rais William Ruto akihudhuria licha ya kuchukuliwa kama mkosoaji mkuu wa vita dhidi ya ufisadi. Dkt Ruto na wandani wake maarufu kama ‘Tangatanga’ hukashifu vita dhidi ya ufisadi wakidai ni njama ya kumvurugia mipango yake ya kushinda urais ifikapo mwaka wa 2022.

Naibu Rais huwa hafichi msimamo wake kwamba vita dhidi ya ufisadi vinafanywa kwa njia isiyofaa, huku viongozi wengine wakidai wapelelezi hulenga tu kukamata wandani wake pekee.

Washirika wa Dkt Ruto wamekuwa hasa wakinyoosha kidole cha lawama kwa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, wakidai ni yeye anayemchochea Rais kuchukua hatua wanazoamini zinataka kumharibia Naibu Rais mipango yake ya kurithi urais ifikapo 2022.

Hii ni licha ya kuwa Bw Odinga na Rais Kenyatta husisitiza kwamba mwafaka wao hauna malengo yoyote ya siasa za 2022. Isitoshe, Rais pamoja na viongozi wanaoegemea upande wake katika chama cha Jubilee, maarufu kama ‘Kieleweke’, hutaka wanachama wote wa Jubilee wawe na msimamo mmoja chini ya uongozi wa Rais.

Juma lililopita, ilifichuka kwamba chama hicho kimepanga kuandaa mkutano mkubwa wa viongozi wake wote mwezi ujao ambapo watasisitiziwa kuhusu hitaji la kufuata maagizo ya chama.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju alisema viongozi wataelezwa wazi kuhusu majukumu yao, mwafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga na mambo ambayo yanaweza kuwafanya waadhibiwe chamani. Kulingana naye, baada ya mkutano huo wanasiasa wanaoenda kinyume na misimamo ya chama wataadhibiwa.

“Tunaandaa mkutano kuwafahamisha kuhusu majukumu yao kwani huwezi kuchukua hatua dhidi ya wanachama ambao hawajui kama kile wanachofanya ni kosa,” alisema.

You can share this post!

Mbunge ndani kwa kumzaba kofi kamanda wa polisi

KPC yaagizwa kuchunguza athari za mafuta yaliyomwagika...

adminleo