• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
STANLEY OLOITIPTIP: Simba wa siasa za Maasai kabla na baada ya uhuru

STANLEY OLOITIPTIP: Simba wa siasa za Maasai kabla na baada ya uhuru

Na KYEB

KUANZIA mwaka wa 1963 na 1983, Stanley Shapashina Ole Oloitipitip alitawala siasa za janibu za Wamaasai kama simba kwani alikuwa na ushawishi mkubwa zaidi enzi hizo.

Itakumbukwa kuwa alipohudumu kama Waziri wa Serikali za Wilaya, Oloitipitip aliipandisha hadhi miji kadha hadi kiwango cha manispaa, hatua ambayo ilipelekea baadhi ya miji hiyo kukumbwa changamoto za kifedha.

Mwanasiasa huyo alizaliwa mnamo 1924 katika eneo la Endoinyo Ootawua karibu na Mlima Kilimanjaro. Oloitipitip alikuwa mtoto wa tatu Mzee Naseramporro Oloitipitip na Mama Olong’oyana Oloitipitip.

Alitoka katika ukoo mdogo wa Irmingana, katika ukoo mkubwa wa Ilatayiok ambao ndio unamiliki Renchi ya Olgulului Ilokarashi iliyoko karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Amboseli.

Alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kajiado Kusini kutokana na sifa zake za kuwa mtetezi sugu dhidi ya mwenendo wa kugawa ardhi ya wamaasai kwa watu kutoka nje. Vilevile, umaarufu wake ulitokana na juhudi zake za kuteta dhidi ya uharibifu wa mali asili na mazingira kwa jumla.

Oloitipitip hakusoma sana kwani alitamatisha masomo yake katika darasa la nne katika Narok Government School ambapo alifanya mtihani wa Kenya African Preliminary Examination mnamo 1941.

Na Vita vya Pili vya Dunia (WWII) vilipoanza, eneo la Kajiado liligeuzwa uwanja wa mapigano huku wanajeshi wa muungano wakipambana na Wanajeshi wa Ujerumani kutoka Tanzania.

Kwa hivyo, Oloitipitip ambaye wakati huo alikuwa mwenye umri wa miaka 19 alijiunga na jeshi la Kings African Rifle (KAR) ambapo alihudumu kama muuguzi msaidizi (nursing orderly). Baadaye aliungana na wanajeshi wa Afrika waliopelekwa katika maeneo ya vita huko Burma, India na Ceylon.

Hakuna habari za kina kuhusu namna Oloitipitip alifanya kazi kama mwanajeshi, japo inadaiwa alipanda ngazi hadi cheo cha sajini kabla ya kurejea nyumbani mnamo 1945 na kuajiriwa tena katika idara ya afya kama daktari msaidizi katika iliyokuwa Wilaya ya Kajiado. Vilevile alimiliki kituo cha afya katika eneo la Il Bissil, Kajiado.

Itakumbukwa kwamba miaka mitano baada ya Oloitipitip kurejea nchini Kenya, siasa za Kenya zilichukua mwelekeo tofauti baada ya Jomo Kenyatta kurejea kutoka Uingereza mnamo Septemba 1946, Vita vya Mau Mau pia vilipoanza huku chama cha Kenya African Union (KAU), chama cha kwanza cha kisiasa chenye ufuasi mkubwa nchini, kilianza kutamalaki.

Baada ya uasi huo wa Mau Mau, Serikali ya mkoloni iliwaendea Wakenya ambao hawakutaka makabila ya Kikuyu, Embu na Meru kuisaidia kupambana na wanapiganaji hao.

Hata hivyo, Oloitipitip kama mwanajeshi za zamani, alikataa kushirikiana na Uingereza katika mpango huo na badala yake akaungana na Waafrika waliokuwa wakipigania uhuru. Vilevile, alifaulu kushawishi watu wa ukoo wake kutoshirikiana na Uingereza kupambana pamoja na wafuasi wa Mau Mau na washirika wao.

Baada ya kufungwa kwa Kenyatta, siasa za Kenya sasa zilihusu mustakabali wa Kenya huku suala la ardhi likipewa uzito. Wazungu walitwaa sehemu kubwa ya ardhi ya Wamaasai na kuigeuza kuwa renchi.

Watu wa jamii yake walifikiria kuunda muungano kwa jina Maasai United Front (MUF), kwa kushirikisha wenzao waliosoma kama Oloitipitip ili kupigania haki haki za jamii ya hiyo.

Bw Oloitiptip ambaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti, aliungana na aliyekuwa mwanahabari wa gazeti la Nation John Keen (aliyechaguliwa kuwa Katibu Mkuu) na Justus Ole Tipis kupigania haki za ardhi za Wamaasai.

Serikali ya Uingereza ilikuwa imependelea sera ya uuzaji na ununuzi wa ardhi baina ya watu wanaokubaliana badala ya mwamko mpya kutoka kwa wenyeji wa kutaka kurejeshwa wa ardhi yao iliyonyakuliwa.

Haki za Wamaasai

Huku chama cha KANU, chini ya uongozi wa James Gichuru na Tom Mboya, kikipendekeza kuwa haki ya kununua ardhi popote iwekwe katika Katiba chini ya Sura kuhusu Haki, chama cha Maasai United Front (MUF) kilitaka kulinda haki za Wamaasai dhidi ya makabila makubwa, haswa Wakikuyu na Waluo. Wanachama wengi wa Kanu walitoka makabila hayo mawili.

Katika wadhifa wake kama mwenyekiti wa MUF, Oloitipitip alikuwa sehemu ya ujumbe wa jamii ya Wamaasai ulioenda kupigania haki za jamii wakati wa Kongamano la Kikatiba jijini Lancaster, Uingereza.

Mnamo Juni 25, 1960 siku chache baada ya kurejea nyumbani kutoka Lancaster, Uingereza, Oloitipitip alifanya mkutano na Masinde Muliro katika ukumbi African District Council, Ngong. Mkutano huo ndio ulibadili siasa za Kenya.

Ilikuwa ni katika mkutano huu, ulioshirikisha baadhi ya vyama vidogo, ambapo chama cha KADU kilibuniwa. Hatua hiyo ilisambaratisha mpango wa kuundwa kwa chama kimoja cha Waafrika, hali ambayo iliyumbisha ubabe wa KANU.

Awali, Bw Muliro ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa KANU iliyoongozwa na Mabw Gichuru na Jaramogi Oginga Odinga, alikuwa ameunda chama cha Kenya African People’s Party. Chama hicho kilishirikiana na kile cha CAPU kilichoasisiwa na Gideon Ngala, chama cha Somali National Association na Kalenjin Politican Alliance katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ngong.

Wanasiasa wengine waliohudhuria mkutano huo walikuwa Daniel Moi, Taita Towett na Francis Khamisi.

Baada ya hapo, Oloitipitip alijitosa ndani ya siasa za KADU na alitangamana na wanasiasa wengine shupavu enzi hizo huku harakati za kutaka uhuru zikishika kasi. Oloitipitip alichaguliwa kuwa Katibu Mratibu wa KADU na ilikuwa katika ngome yake ya Ngong ambapo makabiliano ya kwanza kati ya KANU na KADU yalichipuka mnamo Novemba 1960.

Hii ni baada ya viongozi wa KANU kufika eneo hilo kwa mkutano wao wa kwanza baada ya chama hicho kusajiliwa rasmi. Ni makabiliano hayo yaliyochochea siasa za ardhi katika eneo la Wamaasai na baadaye yakaathiri mwelekeo wa uongozi wa Oloitipitip.

Hatua ya John Keen kuhamia KANU ilipelekea Oloitipitip kuapa kummaliza kisiasa na ndipo akatoa makataa ambayo yalipuuziliwa mbali na Bw Keen.

“Siwatambui wazee ambao wanachukuliwa kuwa vibaraka na ambao hawawezi kukumbatia imani yangu ya kisiasa,” Keen akasema kuashiria kuwa alikuwa ameapa kuasi mrengo wa kisiasa ambao ulikuwa ukiungwa mkono na watu wa jamii yake.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza nchini mnamo Juni 1963, Oloitipitip aliwania kiti cha ubunge cha Kajiado Kusini kwa tiketi ya chama cha KADU, na akaibuka mshindi kwa urahisi. Hapo ndipo alianza maisha yake kama Mbunge yaliyodumu kwa miaka 23 bila kuwahi kushindwa.

Hata hivyo, katika uchaguzi huo, KANU ilitamba kwa kushinda viti 66 kati ya 117 katika Bunge la Wawakilishi na viti 19 kati ya 41 katika Seneti.

Baada ya kushinda ubunge katika uchaguzi huo wa kwanza, Oloitipitip aliibuka kuwa mwanasiasa kutoka jamii ya Wamaasai mwenye hadhi ya juu haswa baada ya John Keen kufeli kutwaa kiti cha Kajiado Kaskazini kwa tiketi ya KANU.

Baada ya Kenya kupata Uhuru mnamo Desemba, Rais Jomo Kenyatta alianza kuimarisha uongozi wake hali iliyopelekea wanachama wa KADU katika mabunge yote mawili kuhamia KANU. Wa kwanza kuvuka sakafu walikuwa Mabw Towett, William Murgor, Jean- Marie Soroney na Oloitipitip. Hali hiyo iliacha KADU chini ya uongozi wa Mabw Moi na Ngala.

Vita vya Oloitiptip na Keen

Wakati huu, hasidi wa kisiasa wa Oloitipitip alikuwa ameteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Siasa za baada ya uhuru katika eneo la Wamaasai zilitawaliwa na vuta nikuvute baina ya Mabw Keen na Oloitipitip kwani walikuwa waking’ang’ania uongozi wa KANU.

Mnamo 1969, Keen aliandaa uchaguzi wa tawi la KANU eneo la Kajiado ambapo wafuasi wote wa Oloitipitip waliondolewa katika nyadhifa zao. Lakini baadaye aliyekuwa Katibu Mkuu wa KANU wakati huo alifutilia matokeo ya uchaguzi huo na kuwarejeshea wandani wa Oloitipitip nyadhifa zao. Wakati huo, Keen alikuwa Katibu Mwandalizi wa KANU ilhali Oloitipitip alikuwa Waziri.

Na katika siasa za kitaifa, Oloitiptip alionekana kulemewa na mawaziri wenye ushawishi mkubwa kutoka uliokuwa Mkoa wa Kati kwani alihudumu kama Waziri wa Mali Asili.

Wakati wa harakati za kubadilisha Katiba (mnamo 1976) kwa lengo la kuzuia Bw Moi, aliyekuwa Makamu wa Rais kumrithi Kenyatta, Oloitipitip aliamua kukabiliana na vizito wa kisiasa walioanzisha msukumo huo. Waliongozwa na vigogo wa Gema kama vile marehemu Njenga Karume, Kihika Kimani na waliokuwa mawaziri Jackson Angaine na Njoroge Mungai.

Oloitipitip aliunga na kundi la wanasiasa waliokuwa wakimuunga mkono Moi ambao walijumuisha aliyekuwa Mkuu wa Sheria Charles Njonjo na G.G Kariuki.

Katika eneo la Pwani, aliyekuwa Waziri Shariff Nassir ndiye aliyejitokeza kupinga kundi la Karume-Kihika- Angaine. Oloitipitip alikusanya sahihi 98, zikiwemo kutoka kwa mawaziri 10, hali ambayo ilimfanya kupendwa na kundi la Njonjo.

Sahihi hizo zilizima uwezo wa kundi hilo la viongozi wa Gema kufaulu kubadilisha Katiba kupitia bunge kwani hawangepata uungwaji mkono kutoka kwa angalau thuluthi mbili ya wabunge wote.

Na zaidi ya hayo Njonjo alizima mjadala kuhusu mabadiliko ya Katiba kwa kutangaza kuwa ilikuwa kinyume cha sheria hata kutafakari kuhusu kifo cha Rais.

Baadaye, Oloitipitip alivuna kutokana na ushirikiano wake na mrengo wa Njonjo kwani aliteuliwa Waziri wa Masuala ya Ndani katika serikali ya kwanza iliyobuniwa na Bw Moi baada ya uchaguzi mkuu wa 1979. Awali, wadhifa huo ulikuwa ukishikiliwa na Makamu wa Rais.

Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Wilaya ambapo aliweza kuongeza idadi ya mabaraza ya miji na manisipaa kwa kupanda hadhi baadhi ya vituo vya kibiashara vijijini.

Bw Moi alianza kukosana na Njonjo baada ya jaribio la mapinduzi la 1982. Wanasiasa wote waliokuwa wandani wa Njonjo wakati huo, akiwemo Oloitipitip walipigwa vita.

Na katika uchaguzi mkuu wa mapema wa 1983, Oloitipitipi ndiye alikuwa mwanasiasa wa kipekee mwandani wa Njojo aliyedumisha kiti chake cha ubunge.

Hata hivyo, Rais Moi hakumpa wadhifa wa uwaziri. Baadaye, Oloitipitip alikamatwa kwa kukiuka sheria za ushuru mnamo 1984 na kufungwa jela kwa miezi 12. Pia alikabiliwa na kosa la kufeli kulipa ushuru kwa Hoteli aliyomiliki katika eneo la Loitokitok kwa jina Maasai Boarding and Lodging.

Baada ya hapo alifukuzwa kutoka KANU na akapoteza kiti chake katika uchaguzi mdogo ambapo Bw Moses Ole Kenah aliibuka mshindi.

Baada ya kutoka gerezani, huku akiugua, Oloitipitip aliamua kujishughulisha na usimamizi wa mali yake, zikiwemo nyumba za makazi katika mtaa wa Lavington Nairobi, kichinjio, hoteli ya kitalii na renchi kadhaa.

Baada kutatiza na unene kupita kiasi, Oloitipitip alifariki katika eneo la Rombo nchini Tanzania mnamo 1985 akiwa na umri wa miaka 61. Alikuwa akitibiwa na daktari wa kienyeji.

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke

You can share this post!

Kaunti kutwaa usimamizi wa kiwanda cha Mumias Sugar

SAKATA YA DHAHABU: Haji aonya wanaosambaza rekodi ya sauti...

adminleo