Habari

Shinikizo serikali ipunguze bei ya unga hadi Sh90 zaanza

May 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

SHIRIKA la kutetea watumizi wa bidhaa limetishia kwenda mahakamani kushinikiza serikali kuweka mikakati ya kupunguza bei ya unga wa mahindi hadi Sh90.

Shirika hilo, Consumer Downtown Association (CDA), linaitaka serikali kurejesha mpango wa unga wa bei nafuu ili kunusuru Wakenya dhidi ya makali ya njaa.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Japheth Ogutu, bei ya juu ya unga na bidhaa nyinginezo muhimu, imesababisha familia nyingi kupata mlo mmoja kwa siku au kulala tumbo tupu.

“Kuanzia Machi, bei ya vyakula humu nchini imekuwa ikiongezeka kwa kasi. Utafiti tuliofanya katika miji yote mikuu kama vile Nairobi, Mombasa, Kisumu, Eldoret na Nakuru ulibaini kuwa bei ya vyakula imeongezeka kwa asilimia 52 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita,” akasema Bw Ogutu.

Alisema kuwa kilo mbili za unga sasa zinazuzwa kwa kati ya Sh120 na Sh150 katika maeneo mbalimbali nchini.

Mnamo 2017, serikali ilitoa Sh6 bilioni kufadhili mradi wa kuagiza mahindi kutoka ughaibuni.

Mpango huo ulisababisha kupungua kwa bei ya kugunia moja la kilo 90 kutoka Sh4,000 hadi Sh2,300. Kupitia mpango huo, bei ya unga wa mahindi ilipungua kutoka Sh153 hadi Sh90 kwa kila kilo 2 za mahindi.

Ripoti ya Shirika la Takwimu nchini (KNBS) ilionyesha kuwa mfumko wa bei ya bidhaa ulivunja rekodi kwa kuongezeka kutoka asilimia 4.35 mnamo Machi hadi asilimia 6.58 mwezi Aprili.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mfumko wa bei ya bidhaa kufikia asilimia 6.58 katika kipindi cha miezi 19 iliyopita.

Mfumko huo wa bei ya bidhaa, kulingana na KNBS, ulisababishwa na ongezeko la bei ya mafuta na hali ya ukame inayoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunaipa serikali makataa ya siku 14 kuweka mikakati ya kupunguza bei ya unga la sivyo tutaenda mahakamani kuishinikiza kufanya hivyo,” akasema Bw Ogutu.

Shirika hilo pia linataka serikali kusitisha mpango wake kuwatoza Wakenya ushuru wa asilimia 1.5 ya mishahara yao.

“Serikali inafaa kufanya utafiti wake ili kuthibitisha ikiwa kweli Wakenya wanahitaji nyumba. Nadhani maelfu ya Wakenya wanahitaji chakula kwa dharura badala ya nyumba,” akasema.