Wataalamu wa ICC kukutana Nairobi kuhusu utafutaji haki
Na VALENTINE OBARA
WATAALAMU wa masuala ya sheria za uhalifu wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali watakutana Nairobi kujadili mbinu bora za utendaji wa haki.
Kongamano hilo litafanyika wakati ambapo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inaadhimisha miaka 20 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Roma ambao ndio msingi wa sheria zake, na pia wakati ambapo utawala wa Jubilee unazidi kushutumiwa kwa kuhujumu uhuru wa mahakama nchini.
Mkutano huo ulioandaliwa na shirika lisilo la serikali la Wayamo Foundation na lile la Africa Group for Justice and Accountability utafanyika kuanzia Februari 27 hadi Machi 2 katika Chuo Kikuu cha Strathmore.
Watakaohudhuria ni wadau wa masuala ya haki kutoka kwa serikali, mashirika yasiyo ya serikali, wasomi, wafanyakazi na wanachama wa mashirika ya kijamii.
Miongoni mwa masuala yaliyopangiwa kujadiliwa ni kuhusu uwajibikaji katika utendaji wa haki kimataifa, barani na kitaifa.
Masuala mengine ni kuhusu uhalifu wa kimataifa, maoni kutoka kwa mahakama na kutoka kwa makundi ya watu walio hatarini zaidi kudhulumiwa kihalifu kama vile watoto na waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi.
Ijumaa iliyopita, maadhimisho ya miaka 20 tangu kubuniwa kwa ICC yalifanywa katika makao makuu ya mahakama hiyo yaliyo The Hague, Uholanzi.
Maadhimisho hayo yalikuwa yaliandaliwa na shirika lisilo la serikali la Coalition for the International Criminal Court.
Waliohutubia maadhimisho hayo walizungumzia mafanikio yaliyopatikana kufikia sasa katika juhudi za kusaka haki kwa waathiriwa wa uhalifu wa kimataifa na changamoto zilizopo, huku wito ukitolewa kuimarisha mfumo wa utendakazi katika mahakama hiyo.
Umuhimu wa haki
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw António Guterres, alisema kwamba maadhimisho hayo yametoa nafasi kwa wadau wote kutafakari kuhusu umuhimu wa haki katika kudumisha amani, usalama na kutetea haki za kimataifa.
“Hakuwezi kukawa na matumaini ya kuzuia uhalifu na kudumisha amani katika siku za usoni iwapo wahusika wa uhalifu wa aina hizo hawatashtakiwa na kuadhibiwa,” akasema.
Wengine waliohutubu ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Bw Kofi Annan, Rais wa ICC, Jaji Silvia Fernández de Gurmendi, Kiongozi wa Mashtaka katika mahakama hiyo, Bi Fatou Bensouda na Balozi wa Mashauri ya Kigeni katika Muungano wa Ulaya, Bi Federica Mogherini miongoni mwa wengine.
“Sote tunafahamu kuwa tunaelekea katika kipindi chenye misukosuko zaidi ulimwenguni. Ushirikiano wa mataifa ambao ulisaidia kufanikisha kubuniwa kwa mahakama hii uko hatarini,” akasema Jaji Gurmendi.
Mahakama hiyo ilikashifiwa vikali na viongozi wa Afrika wakati wa kesi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.