Michezo

Ilinikata maini kubanduliwa UEFA, afunguka Gundogan

May 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

KIUNGO wa Manchester City Ilkay Gundogan amesema kwamba kubanduliwa kwenye ligi ya mabingwa UEFA kulimkata maini.

“Kubanduliwa kwenye ligi ya mabingwa kulikuwa uchungu sana. Hata hivyo ni kazi bure kulilia hilo ilhali tumeshinda mataji matatu nyumbani. Kila ambacho nalenga katika siku za usoni ni kushinda Uefa,” akasema Gundogan.

Kiungo huyo yupo tayari kuanzisha mazungumzo na Manchester City ili kurefusha kandarasi yake ugani Etihad hasa baada ya kutwaa mataji matatu msimu uliokamilika wa 2018/19.

Gundogan yupo kwenye mkondo wa lala salama katika kandarasi yake na amekuwa akiaminiwa na kocha Pep Guardiola kikosini kwa kuwa amesakata mechi 31 za Ligi Kuu ya Uingereza msimu uliokamilika wa 2018/19 hasa kutokana na Fernandinho na Kevin De Bruyne kuuguza majeraha ya mara kwa mara.

“Sasa ni wakati wa kuangazia jinsi mambo yalivyo na kuhusisha klabu kwenye mazungumzo ya kurefusha kandarasi yangu,” akasema Gundogan ambaye alijiunga na Manchester City kutoka Dortumund ya Ujerumani misimu mitatu iliyopita.

Ingawa City iliandikisha historia nchini Uingereza kwa kushinda mataji matatu, Guardiola amedai mara kwa kipindi atakachohudumu kama kocha kitategemea ufanisi wake katika kipute cha Klabu Bingwa Barani Ulaya(Uefa).

Manchester City walibanduliwa katika Uefa msimu huu na Tottenham ambao watakutana na Liverpool kwenye fainali ya Uefa Julai 1 katika uga wa Juventus nchini Italia.